Oct 26, 2021 02:30 UTC
  • Wiki ya Umoja na vizingiti vinavyozuia kupatikana umoja wa nchi za Kiislamu

Tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal sawa na tarehe 19 hadi 24 Oktoba zimetengwa na kutangazwa rasmi kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na Jumapili ya juzi ndiyo iliyokuwa siku ya mwisho ya wiki hiyo muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Nchi za Kiislamu zina mambo mengi yanayofanana na yanayozipa uwezo wa kuimarisha umoja na mshikamano wao. Mbali na suala la Uilsmau nchi hizo zina mambo mengine mengi yanayofanana zikiwemo lugha ambazo zinaweza kuzifanya kuwa kitu kimoja. Nyingi ya nchi hizo zina mambo mengi yanayofanana kiutamaduni, kisiasa na kijamii na kwa kawaida zinapasa kuwa na uhusiano mzuri. Pamoja na hayo umoja unaohitajika hauonekani popote kati ya nchi hizo jambo linaloibua swali kwamba je, ni kwa nini kuna hitilafu na uhusiano mbaya kati ya nchi za Kiislamu licha ya kuwepo mambo hayo yote yanayopasa kuziweka pamoja?

Katika kujibu swali hili muhimu tubapasa kuzingatia baadhi ya masuala ya ndani na nje ya mipaka ya nchi hizo.

Katika uwanja wa ndani kuna baadhi ya mambo ambayo yanazua hitilafu kati ya nchi za Kiislamu. Kwa mfano katika baadhi ya nchi kuna miundo hasimu ya kikabilia ambayo kwa kawaida huibua hitilafu na kuweza kutumiwa vibaya na maadui kwa ajili ya kufikia malengo yao haramu na yaliyo dhidi ya Uislamu katika nchi hizo.

Suala hilo linaonekana wazi katika nchi za Iraq, Bahrain, Saudi Arabia na Uturuki. Mbali na hayo, miundo ya kiutawala katika baadhi ya nchi hizo ambayo kwa kawaida ni kandamizi na wala mambo kama demokrasia na haki za binadamu hayana umuhimu mkubwa kwa watawala wa nchi hizo, ni suala linaloyakandamiza makundi ya wachache kidini na kikabila, na wakati huo huo kuzifanya nchi zilizo na uwezo wa kijeshi kuvamia na kuzichokosa nchi nyingine jirani zilizo na uwezo mdogo katika uwanja huo.

Kuhusu sababu za nje, siasa za madola makubwa ndiyo sababu kuu inayozuia nchi za Kiislamu kuwa na umoja. Baadhi ya mivutano ya ndani ambayo inaoonekana katika nchi za Kiislamu pia inatokana na siasa za kikoloni zilizotekelezwa katika nchi hizo katika karne zilizopita na madola ya Magharibi na hasa Uingereza. Madola hayo yalitekeleza na yangali yanatekeleza siasa hizo za kugawanya na kuibua mifarakano katika nchi za Kiislamu ili yapate kuzitawala na kudhibiti vyanzo vya utajiri wao asilia.

Kuibua na kuchochea mambo kama hitilafu za Shia na Suni, Waarabu na Waajemi, Waarabu na Wakurdi, Wafursi na Waturuki au Waarabu na Waturuki hayo yote ni katika mbinu na siasa zinazotumiwa na madola ya kikoloni ya Magharibi kwa ajili ya kuibua hitilafu na mifarakano kati ya nchi za Kiislamu. Baadhi ya nchi za Kiislamu pia zimetumbukia katika mtego huo wa Wamagharibi na zinashirikiana nao kwa ajili ya kupora mali na kuharibu dini na utamaduni wa Waislamu.

Suala jingine ni kuwa madola ya Magharibi yanaamini kuwa yanaweza tu kudhibiti hali ya mambo katika eneo muhimu na la kistratijia la Asia Magharibi kwa kuibui mifarakano na mivutano kati ya nchi za eneo. Yanaamini pia kwamba kuwepo umoja na mshikamano wa nchi za Kiislamu kunaweza kupelekea nchi hizo kuimarika zaidi kinguvu na hivyo kuwa na usemi wa mwisho kuhusu masuala muhimu ya kieneo na hata ya kimataifa. Ni kutokana na ukweli huo ndipo yakawa yanatumia gharama kubwa kwa ajili ya kuendeshea propaganda za kuzuia kupatikana umoja wa nchi za Kiislamu. Katika ujumbe wake kwa kikao cha kimataifa cha 35 cha Umoja wa Kiislamu, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Chama cha Hizbullah cha Lebanon amesisistiza umuhimu wa Waislamu kuimarisha umoja na mshikamano wao na kuongeza kuwa: "Wakati Waislamu wa Kishia na Kisuni walipoamua kushirikiana bega kwa bega katika mapambano waliweza kuishinda Daesh, katika hali ambayo maadui ambao wanataka kutudhibiti katika eneo wanataka tupigane sisi kwa sisi."

Suala jingine muhimu ni kwamba umoja na mshikamano wa nchi za Kiislamu unahatarisha maslahi na usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Madola ya Magharibi yametangaza wazi kuwa kuulinda utawala huo kwa hali na mali ni moja ya majukumu yao makuu na bila shaka umoja wa nchi za Kiislamu unakinzani na majukumu hayo.

Kwa kutilia maanani ukweli huo tunaweza kusema kuwa sababu za nje zinazotokana na siasa za madola makubwa ya Magharibi ndicho kizuizi kikuu katika njia ya kupatika umoja wa nchi za Kiislamu. Ni wazi kuwa madola ya kibeberu ya Magharibi yameamua kusimama imara kwa ajili ya kukabiliana kwa kila mbinu na juhudi zozote za kupatikana umoja na mshikamano katika nchi za Kiislamu.

Tags