Oct 27, 2021 13:00 UTC
  • Wanaharakati wa kulinda mazingira walemaza shughuli zote mashariki na magharibi ya London, Uingereza

Wanaharakati wa kulinda mazingira wamelemaza na kukwamisha shughuli mbalimbali katika maeneo mawili ya mashriki na magharibi ya mji mkuu wa Uingereza, London baada ya kufanya mgomo wa kuketi wakilalamikia hali ya mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka joto la sayari ya dunia.

Wanachama wa harakati ijulikanayo kama Insulate Britain leo wamefanya mgomo wa kuketi katika barabara kuu ya A40 iliyoko magharibi mwa London huku kundi jengine la wanaharakati hao likipiga kambi kwenye barabara kuu ya M25 karibu na kivuko cha eneo la Dartford na kuweka kizuizi kwa magari yaliyohitaji kupita katika barabara hiyo.

Katika kipindi cha majuma sita yaliyopita kundi hilo la wanaharakati wa kulinda mazingira limekuwa likifanya mgomo wa kuketi katika barabara kuu kadhaa na zenye msongamano mkubwa wa magari mjini London na kusababisha mkwamo wa magari, ambapo wanachama wapatao 700 wa harakati hiyo wamekamatwa na polisi na kupewa onyo la kuchukuliwa hatua za kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Wanaharakati wa Insulate Britain wakiwa katika mgomo wa kuketi

Harakati ya Insulate Britain ni moja ya matawi ya Kundi la Mapambano Dhidi ya Utowekaji linalotaka zichukuliwe hatua za haraka kushughulikia hifadhi ya mazingira.

Mbali na kutaka itangazwe rasmi hali ya hatari, wanaharakati hao wanataka serikali ya Uingereza ipitishe sheria itakayolazimisha kudhibitiwa ongezeko la gesi chafu ya dioksidikaboni na kuhakikisha gesi hiyo inapunguzwa na kufikia kiwango cha sifuri ifikapo mwaka 2025.

Aidha wanataka serikali ihakikishe majengo yote nchini humo yanakuwa na mfumo wa udhibiti joto utakaozuia ueneaji wa gesichafuzi ya greenhouse.

Wiki ijayo Uingereza itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa tabianchi utakaofanyika mjini Glasgow kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi mbalimbali za dunia.../

Tags