Nov 06, 2021 15:47 UTC
  • Serikali ya Biden yaidhinisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani imeidhinisha mauzo ya makombora yenye thamani ya dola milioni 650 kwa Saudi Arabia.

Washington imedai kuwa, mauzo ya makombora hayo kwa Saudia yatasaidia kwa ajili ya kujilinda mbele ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kutoka nje zinazolenga maafisa wa kijeshi wa Saudia na Marekani.

Wakati huo huo Shirika la Wakala wa Ushirikiano wa Usalama wa Ulinzi wa Marekani (DSCA) limeitaarifu Kongresi ya nchi hiyo kwamba, mauzo ya silaha hizo kwa Saudia yataimarisha siasa za kigeni na usalama wa kitaifa wa Marekani. Barua ya DSCA imeitaja Saudi Arabia kuwa ni "nchi rafiki" inayohesabiwa kuwa "nguvu muhimu kwa ajili ya matukio ya kiuchumi na kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati".

Mauzo ya silaha mpya za Marekani kwa Saudia ni kinyume na ahadi ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo ya kukomesha vita vya Yemen na kuzuia uuzaji wa silaha za kuhujumu kwa utawala wa Riyadh. 

Marekani yaidhinisha mauzo ya silaha kwa Saudia

Utumiaji wa silaha za Marekani dhidi ya maeneo ya raia nchini Yemen unakosolewa sana na watetezi wa haki za binadamu. Ili kuhalalisha hatua hiyo, serikali ya Biden imedai kuwa makombora hayo hayatatumiwa kulenga shabaha za ardhini. 

Licha ya madai ya hapo awali ya serikali ya Biden ya kutazama umpya uhusiano wa Washington na Riyadh na kuwa na msimamo mkali kuhusiana na utawala wa Aal Saud lakini inaonekana kuwa maslahi ya muda mrefu na ya jiografia ya kisiasa ya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia yameifanya Washington ibadili msimamo wake kuhusu Saudia. Baada ya Biden kushika madaraka ya nchi Januari mwaka huu wa 2021 na kwa kutilia maanani misimamo ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali yake kama Antony Blinken ilitarajiwa kuwa, kutafanyika mabadiliko makubwa katika uwanja huo. Hata hivyo sasa imebainika kuwa, siasa kuu za Marekani kuhusu Saudia ambayo ni mshirika mkuu wa nchi hiyo katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Magharibi mwa Asia kwa ujumla, ni kuunga mkono na kuuhami kwa pande zote utawala huo wa kifalme. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana serikali ya Biden imeendelea kutoa misaada na ushirikiano wa kijeshi kwa utawala huo. 

Mtaalamu wa masuala ya siasa za nchi za Kiarabu, Taha Al-Ani anasema: "Japokuwa serikali ya Biden imekua na siasa tofauti kuhusiana na Saudia ikilinganishwa na ile ya Donald Trump na imefanya jitihada za kutazama upya uhusiano wake na nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi, lakini mazoezi ya kijeshi baina ya Washington na Riyadh bado hayajasimamishwa.”

Serikali ya Biden ilitangaza kuwa itasimamisha mauzo ya silaha za kuhujumu kwa Saudi Arabia kutokana na vita vya nchi hiyo huko Yemen. Sasa Biden imechukua hatua ya kuimarisha zaidi uwezo wa kijeshi ya Saudia kwa kisingizio kwamba, Yemen inashambulia ardhi ya nchi hiyo. Hatua hiyo ya Marekani ya kulegeza msimamo na kurudi nyuma kimyakimya imechukuliwa baada ya Biden kutangaza kwamba: “Marekani kamwe haitaacha misingi yake nyuma ya mlango kwa ajili tu ya kununua mafuta na kuuza silaha.”

Joe Biden

Sasa imebainika kuwa matamshi hayo ya Biden yalikuwa changa la macho. Kwa msingi huo na kwa kutumia kisingizio cha kukabiliana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za wanamapambano wa Yemen na kulinda taasisi na vituo vya mafuta na vya kistratijia, Wasaudia wameomba kuuziwa silaha za kisasa za Marekani au kwa maneno mengine kukarabati uhusiano wa Riyadh na Washington. Hatua ya serikali ya Biden ya kukubali ombi la Saudia inaonesha kuwa, Marekani imepuuza kabisa majanga na maafa makubwa yanayoendelea kufanyika nchini Yemen kwa kipindi cha miaka sita kutokana na mashambulizi ya Saudi Arabia na waitifaki wake wengine kama Imarati, na badala yake imefadhilisha maslahi na malengo yake ya kisiasa na kiuchumi.    

Tags