Nov 11, 2021 09:46 UTC
  • Xi Jinping
    Xi Jinping

Rais Xi Jinping wa China ameonya kuhusu uwezekano wa kurejea mgogoro wa zama za Vita Baridi katika eneo la Asia Pasifiki huku hali ya taharuki ikiendelea kushuhudiwa baina ya Marekani na China kuhusu eneo la China Taipei.

Akihutubu pembizoni mwa kongamano la viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kibiashara Asia-Pasifiki (APEC) huko New Zealand, Xi Jinping amesema njama za kuibua migawanyiko ya kiaidiolojia au kuunda makundi madogo madogo katika uga wa jiografia ya kisiasa zitafeli. Amesema eneo la Asia-Pasifiki haliwezi kurejea tena katika zama za makabiliano yaliyokuwepo wakati wa Vita Baridi.

Matamshi ya Xi yanaonekana yalielekezwa kwa muungano unaoongozwa na Marekani wa India-Pasifiki kwa lengo la kupunguza ushawishi wa kiuchumi na kijeshi wa China.

Serikali ya China imejibu matamshi yaliyotolewa majuzi na Rais Joe Biden wa Marekani kuhusu Taiwan na kumtaka awe na tahadhari zaidi. Beijing imesisitiza kuwa, haitalegeza kamba wala kufanya suluhu kuhusiana na masuala ya kimsingi kama mamlaka yake na mipaka ya ardhi ya nchi hiyo.

Image Caption

Hivi karibuni Rais Joe Biden wa alisema kuwa, iwapo jeshi la China litaishambulia Taiwan basi Marekan itakuwa tayari kukilinda kisiwa hicho. Wakati huo huo mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa ameitahadharisha serikali ya Washington isije ikakitumbukiza kisiwa hicho katika vita.

China inaitambua Taiwan kuwa ni sehemu ya ardhi ya nchi hiyo na inafanya mikakati ya kukiunganisha tena na ardhi mama kupitia sera za China Moja na Mifumo Miwili kama ilivyofanya kuhusiana na Hong Kong na Macao. Hata hivyo Marekani ambayo miaka ya karibuni imepatwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na kuporomoka ushawishi wake duniani kutokana na kasi ya ustawi na maendeleo ya China, imezidisha sana mashinikizo dhidi ya Beijing kupitia njia ya kustawisha zaidi ushirikiano wake na Taiwan na kuzidisha uwezo wake wa kijeshi mkabala wa China. 

Tags