Nov 12, 2021 02:23 UTC
  • Baraza la Usalama lataka kuhitimishwa ukandamizaji dhidi ya raia nchini Myanmar

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa inayoelezea wasiwasi mkubwa kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Myanmar, ambapo wanajeshi waliotwaa madaraka ya nchi wanafanya ukandamizaji dhidi ya wapinzani na kutoa wito wa kuhitimishwa vitendo hivyo.

Nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimetoa taarifa hiyo na kusisitiza kwamba, jeshi la Myanmar linapaswa kuhitimisha vitendo vya ukandamizaji dhidi ya raia wanaopinga utawala wa kijeshi.

Aidha taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataita imewataka wanajeshi wanaotawala nchini humo kutayarisha mazingira ya upelekwaji misaada na kufikiwa raia wanaohitajia misaada ya kibinadamu nchini Myanmar.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, makundi ya wanaharakati nchini Myanmar yamesema watu zaidi ya elfu moja wameuawa tangu yalipojiri mapinduzi ya kijeshi nchini humo mwezi Februari mwaka huu.

Maandamano ya wananchi wa Myanmar ya kupinga utawala wa kijeshi

 

Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.

Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai ya kutokea wizi na udanganyifu katika uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana ambapo chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.

Tangu wakati huo, kumekuwa kukishuhudiwa maandamano ya wananchi na makundi mbalimbali ya kiraia ya kupinga hatua ya jeshi ya kufanya mapinduzi na kutwaa madaraka ya nchi.

Tags