Nov 13, 2021 11:49 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakosoa vitendo vya mabavu vya nchi za Ulaya dhidi ya wakimbizi

Akizungumza katika bunge la Ulaya Filippo Grandi Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amekosoa vitendo vya mabavu na ukandamizaji wa Umoja wa Ulaya dhidi ya wakimbizi na kusisitiza kuwa siku zote na mara kwa mara tunashuhudia raia wanaotafuta hifadhi barani Ulaya wakifukuzwa kwa mabavu na visingizio vya kisheria kutumika katika kuwanyima hifadhi raia hao.

Amesema Umoja wa Ulaya ni taasisi inayofuata utawala wa sheria na kwa msingi huo inapasa kuwajibika ipasavyo katika uwanja huo. Kamisha Mkuu wa UNHCR ameutuhumu pia Umoja wa Ulaya kuwa unakiuka sheria katika kuamiliana na wakimbizi na raia wanaotafuta hifadhi na kuongeza kuwa katika baadhi ya maeneo tumeshuhudia wakimbizi wakifukuzwa na kurejeshwa walikotoka huku wakipigwa na kuteswa. 

Wakimbizi katika mpaka wa Poland na Belarusia 

Amesema, raia wanaotafuta hifadhi na wahajiri wakati mwingine huvuliwa nguo na kutupwa mtoni au kuachwa peke yao ili wazame baharini.  

Inaonekana kuwa hotuba hiyo ya afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa imezilenga hasa Poland, Italia na Ugiriki; ambazo zinapatikana katika mipaka ya Umoja wa Ulaya mashariki na kusini mwa bara hilo.  

Hatua ya Umoja wa Mataifa ya kukosoa vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofanyiwa wakimbizi na nchi za Ulaya imechukuliwa katika kivuli cha matukio ya hivi karibuni khususan matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika mipaka ya Poland na Belarusia. Ndio maana Grandi ameashiria hali ya maafa inayowakabili wakimbizi katika mpaka wa Poland bila ya kutaja jina la nchi husika. Amesema ni jambo lisilokubalika kuona serikali zikiwalazimisha watu walioko katika mazingira ya hatari kufanya safari hatarishi. 

Inaonekana kuwa Filippo Grandi aliikusudia wazi Belarusia ambayo imewachochea wakimbizi kuelekea upande wa mipaka ya Poland na Lithuania. Nchi mbili hizo yaani Poland na Lithuania zimetangaza hali ya hatari kufuatia kuongezeka idadi ya wakimbizi kutoka Belarusia. Ripoti zinasema karibu wakimbizi elfu mbili hadi nne wamekwama katika maeneo ya mpakani kati ya Poland na Belarusia. Aidha nchi mbili hizo zimetuma wanajeshi katika maeneo hayo ya mpakani ili kukabiliana na wimbi hilo la wakimbizi.   

Ni wazi kuwa, wakimbizi hao wamelazimika kuelekea upande wa mpaka wa Poland kutokana na mashinikizo ya kikosi cha ulinzi wa mpakani cha Belarusia; na katika upande mwingine ni kuwa, wakimbizi hao hawakuwa na njia nyingine mbadala kutokana na ukandamizaji na vitendo vya mabavu walivyokumbana navyo kutoka kwa askari ulinzi wa mpakani wa Poland na hivyo kuwafanya wakwame katika maeneo ya mpaka wa nchi mbili hizo huku wakikabiliwa na hali ngumu. 

Poland imetangaza hali ya hatari  katika maeneo ya mpaka wake na Belarusia tangu tarehe pili mwezi huu wa Novemba na hivyo kuyazuia mashirika ya haki za binadamu na waandishi wa habari kuingia katika maeneo hayo. 

Polisi wa mpakani wakiwa mbele ya watafuta hifadhi katika mpaka wa Poland na Belarusia 

Katika wiki za hivi karibuni Warsaw pia imetuma katika maeneo hayo ya mpakani maelfu ya askari usalama na wanajeshi na kuimarisha ulinzi kwa kujenga uzio wa muda kando kando ya mipaka hiyo tajwa. Wakati huo huo licha ya hitilafu kubwa zilizopo kuhusu namna ya kuamiliana na wakimbizi barani Ulaya lakini Charles Michel Mkuu wa Baraza la Ulaya ametangaza kuwa yuko pamoja  kikamilifu  na Poland katika uwanja huo. Amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya unapasa kutoa jibu la pamoja kwa sera za Belarusia kufuatia hatua yake ya kuwatuma wakimbizi katika mipaka ya Umoja wa Ulaya. Ni wazi kuwa, wakimbizi wanatumiwa kama wenzo wa makabiliano kati ya Belarusia na Umoja wa Ulaya. 

Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya 

Gerald Knaus mchambuzi mtajika wa masuala ya wakimbizi na mwanasosholojia wa Magharibi ameashiria kujiri mgogoro mkubwa zaidi wa kimaadili wa Umoja wa Ulaya katika mipaka yake katika miaka ya karibuni na kueleza kuwa, umoja huo umeanzisha maonyesho ambapo umepuuza sheria na kanuni zake zote."   

Licha ya hali ya sasa waliyonayo raia wanaotafuta hifadhi katika mpaka wa Belarusia na Umoja wa Ulaya, ambao wanakabiliwa na hali mbaya na vitendo visivyo vya kibinadamu lakini tukitupia jicho uwajibikaji wa akthari ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya tangu kuibuka mgogoro wa wakimbizi tunaona kuwa, nchi za Ulaya hazijawajibika na kukubali majukumu mkabala wa wakimbizi na wahajiri bali zimekuwa zikiamiliana na watu hao kwa njia isiyo ya kibinadamu. Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Ulaya siku zote unadai kuwa mtetezi wa haki za binadamu duniani na wakati huo huo kutoa madai chungu nzima katika uwanja huo dhidi ya nchi zinazopinga umoja huo wa Magharibi.

Tags