Nov 18, 2021 07:45 UTC
  • Marekani yaweka rekodi mbaya mpya; mara hii ni ya vifo vinavyotokana na madawa ya kulevya

Kituo cha udhibiti na uzuiaji maradhi cha Marekani kimetangaza kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, takwimu za vifo vinavyosababishwa na matumizi ya kupindukia ya madawa ya kulevya zimevuka kiwango cha watu laki moja kwa mwaka.

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa, data za awali za kituo cha kuzuia na kudhibiti maradhi cha nchi hiyo zimeonyesha kuwa, katika kipindi cha miezi 12 iliyoishia mwezi Aprili mwaka huu wa 2021 takwimu za vifo vilivyotokana na utumiaji wa kupindukia wa mihadarati nchini Marekani zimeongezeka kwa asilimia 29 na kufikia 100,306.

Inasemekana, mihadarati ya kemikali na ya viwandani ikiwemo ya aina ya fetanyl inasababisha karibu asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na matumizi ya kupita kiasi ya madawa ya kulevya nchini Marekani.

Baada ya kurejea hali na mazingira ya kabla ya janga la corona, wataalamu wanasema, ikiwa hazitachukuliwa hatua za kuboresha kwa kiwango kikubwa utoaji huduma za tiba, Wamarekani wataendelea kupoteza maisha kwa matumizi ya kupindukia ya mihadarati na vichangamsho vyenye nguvu kubwa.../

Tags