Nov 19, 2021 02:53 UTC
  • Russia yakosoa mwenendo wa kinafiki wa Marekani kuhusu masuala ya anga

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amezitaja tuhuma za Marekani dhidi ya Moscow kwamba inatumia silaha dhidi ya satalaiti na kusababisha vitisho angani kuwa ni za kinafiki na zisizo na ukweli wowote. Sergey Lavrov amesema kuwa: "Tunaona kwkamba, badala ya kutoa madai yasiyo na msingi wowote, ni vyema Marekani iketi kwenye meza ya mazungumzo na ieleze mitazamo yake kuhusu makubaliano yaliyopendekezwa na Russia na China kwa ajili ya kuzuia mashindano ya silaha angani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza hayo akimjibu Antony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani aliyeikosoa Russia kwa kulifanyia majaribio kombora lake dhidi ya satalaiti. Antony Blinken alisema katika taarifa yake kwamba Russia Jumatatu tarehe 15 mwezi huu, bila ya kuchukua tahadhari yoyote, ilifanya jaribio lenye uharibifu la kombora lake dhidi ya satalaiti lililolenga moja ya satalaiti zake angani. Vilevile Ned Price Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani na John Kirby ambaye msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) kwa upande mmoja na Ben Wallace Waziri wa Ulinzi wa Uingereza kwa upande wa pili wamelaani hatua hiyo ya Russia.  

Antony Blinken, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Katika mashindano ya anga yanayoendelea sasa kati ya Russia na China kwa upande mmoja, na Marekani katika upande wa pili, pande zinazovutana zinatuhumiana kwa kusema uwongo na kuwa na mienendo ya kinafiki. Pamoja na hayo, tukitupia jicho hatua na mipango ya anga ya nchi tatu hizo tunaona kuwa, Washington inafuatilia mikakati kabambe ili kuwa na udhibiti katika masuala ya anga; na hatua zinazotekelezwa na Russia na China katika uwanja huo bila shaka ni jibu kwa harakati za anga za Marekani.  

Marekani imechukua hatua kubwa katika kuimarisha uwezo wake wa anga tangu kipindi cha utawala rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump. Mwezi Juni 2018 Trump aliiamuru Pentagon iunde kikosi cha anga kama sehemu ya matawi ya vikosi vya ulinzi vya Marekani. Kikosi hicho cha anga cha Marekani kilianza kazi rasmi mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka 2019. Baada ya kuanza kazi, Washington ilichukua hatua kubwa za kuingiza sera za kijeshi katika sekta ya masuala ya anga. Kwa msingi huo Pentagon iliandaliwa uwanja wa kujiimarisha, kufanya majaribio na kutuma silaha angani hususan silaha dhidi ya makombora zikiwemo silaha za leza baada ya kuanza kazi kamandi ya masuala ya anga ya nchi hiyo. 

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump  

Katika kuhalalisha hatua zake hizo, Washington ilidai kuwa, vitisho vya anga vya maadui wa Marekani, hususan Russia na China, vimeongezeka katika miaka ya karibuni na kwamba nchi hizo zinataka kutuma silaha za kivita angani.   

Cecil Eugene Diggs Haney, admirali mstaafu wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani ambaye aliwahi kuwa Kamanda wa Kikosi cha Kimkakati ya Marekani (STRATCOM) anasema: Marekani inapasa kujifunza zaidi kuhusu nguvu na uwezo unaoweza tarajiwa wa maadui na wakati huo huo izidishe bajeti ya mipango yake ya anga na kujiandaa kikamilifu.

Hatua kubwa zinazotekelezwa na Marekani katika uga wa anga  zimekosolewa vikali na wapinzani wa nchi hiyo. Russia imeikosoa Marekani kuhusu suala hilo na kueleza kuwa, makabiliano ya kijeshi angani yanaweza kuwa na hatari sawa na mashindano ya silaha za nyuklia, na imeitaka Washington kutorudia makosa ya huko nyuma.

Inaonekana kuwa, lengo la Marekani ni kuwaingiza katika mashindano ya kijeshi na ya silaha mahasimu wake wakuu yaani Russia na China. Mwaka 2014 Russia iliwasilisha kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa muswada wa kuzuia utumaji silaha angani, ambao hata hivyo ulikabiliwa na upinzani wa Marekani na waitifaki wake. Moscow imekosoa kuendelea upinzani wa Washington dhidi ya pendekezo hilo na kusema, muswada huo umepingwa ili kutimiza mipango ya Marekani ya kutuma silaha angani.

Katika kuthibitisha kuwa ni dola lenye nguvu kubwa za kijeshi duniani, Marekani inajaribu kuibadili anga ya dunia kuwa sehemu ya shughuli zake za kijeshi; hatua ambayo mwishowe itazidisha ukosefu wa amani na kudhoofisha usalama wa dunia. 

Tags