Nov 19, 2021 07:47 UTC
  • Ripoti: Mihadarati inaua watu zaidi ya laki 1 kila mwaka Marekani

Ripoti mpya ya utafiti inaonesha kuwa, idadi ya watu wanaopoteza maisha kutokana na matumizi ya mihadarati nchini Marekani imeongezeka na kupindukia watu laki moja kwa mwaka.

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Marekani CDC kimetoa taarifa hiyo na kueleza kwamba, watu wengi zaidi wanakufa kila mwaka kutokana na matumizi ya dawa za kulevya kuliko wale wanaoaga dunia kutokana na kupigwa risasi au na ajali za barabarani. 

Idara hiyo imesema matumizi ya mihadarati yameongezeka kwa asilimia 28.5 kati ya mwezi Mei mwaka 2020 hadi mwezi Aprili mwaka huu wa 2021.

Mkurugenzi wa Kitaifa wa Kudhibiti sera ya Dawa za Kulevya nchini Marekani Dr. Rahul Gupta amesema hali hii isiyo ya kawaida haikubaliki na inahitaji kutafutatiwa majibu ya haraka.

Wataalamu nchini humo wamesema aktari ya vifo hiyvo vimetokana na matumizi ya dawa ya kulevya aina ya Fentanyl, huku baadhi ya watumiaji wakiichanganya na mihadarati aina ya heroin, cocaine, au methamphetamine.

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni wa Gall Up ni kwamba, asilimia 64 ya Wamarekani wanataka kuona bangi 'ikihahalishwa' kote nchini. Takwimu zinazonesha kuwa, takribani asilimia 70 ya wananchi wa Marekani wametumia bangi japo mara moja katika kipindi cha maisha yao. 

Matumizi ya mihadarati nchini Marekani yanaisababishia nchi hiyo hasara ya dola bilioni 740 kila mwaka, mbali na kuchangia pakubwa ongezeko la vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani nchini humo.

Tags