Nov 21, 2021 02:51 UTC
  • Wakati utawala haramu wa Israel unapomnyooshea mkono 'baba wa ubatizo'

Ijumaa iliiyopita serikali ya Uingereza ikiwa baba wa ubatizo wa mwanaharamu wake katika eneo la Magharibi mwa Asia (Israel) iliendeleza siasa na sera zake za kihasama na kiadui dhidi ya taifa la Palestina kwa kuitangaza harakani ya kupigania ukombozi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu HAMAS kuwa ni kundi la kigaidi.

Baada ya hatua hiyo ya London, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Priti Sushil Patel, alipiga marufuku shughuli zote za harakati ya Hamas nchini humo. Uamuzi huo wa Uingereza ikiwa nchi iliyotayarisha mazingira ya kuporwa ardhi ya Palestina kwa kutoa Azimio la Balfour (Balfour Declaration) mwaka 1917 lililoikabidhi ardhi ya Palestina kwa Wazayuni maghasibu, umekabiliwa na upinzani mkubwa. Kama ilivyotarajiwa, Israel imekaribisha na kupongeza uamuzi huo. Waziri Mkuu wa utawala huo haramu, Naftali Bennett na Waziri wake wa Mambo ya Nje Yair Lapid wamepongeza uamuzi huo wa serikali ya Uingereza. Lapid ameutaja uamuzi huyo kuwa ni "mafanikio mengine ya wizara ya mambo ya nje ya utawala huo. 

Azimio la Balfour

Tunapotazama kwa undani hatua hiyo tunaweza kuutaja uamuzi wa Uingereza kuwa ni radiamali (reaction) dhidi ya mafanikio ya miaka ya karibuni ya harakati za kupigania uhuru katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi huko Palestina. Kwa maneno mengine ni kuwa, uamuzi huo wa serikali ya Landon ni jibu la hasira na ghadhabu la 'baba wa ubatizo' kutokana na kushindwa mtawalia kwa mwanaharamu, Israel, na vitisho va uwepo na mustakbali wa utawala huo ghasibu na bandia. Kwa msingi huo Uingereza imeamua kukanyaga nara zake tupu za eti kutetea haki za binadamu na kuitangaza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS, inayotambuliwa na mataifa yote ya Mashariki ya Kati na asasi nyingi za kimataifa, kuwa ni kundi la kigaidi! Kwa uamuzi huo, London imeonesha kwa mara nyingine kwamba, ni wenzo unaotumiwa na lobi na makundi ya mashinikizo ya Wazayuni kutimiza malengo yao. Hatua hii imechukuliwa pia kusitisha au kuzuia kufeli na kushindwa zaidi serikali ya sasa ya Israel na ni kielelezo cha matatizo ya kiusalama yanayozidi kuuzonga utawala huo haramu. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Yair Lapid akaitaja kuwa ni "ushindi na mafanikio mapya". 

Harakati ya Hamas kwa upande wake, imetoa taarifa ikisema, serikali ya Uingereza ilipaswa kuona aibu kutokana na mchango wake katika kuasisiwa utawala haramu wa Israel katika ardhi ya Palestina. Hamas imesisitiza kuwa: "Badala ya kuomba radhi na kurekebisha makosa yake ya kihistoria dhidi ya watu wa Palestina kupitia Azimio la Balfour na kuikabidhi ardhi ya Wapalestina kwa makundi ya Kizayuni wakati ilipokuwa ikisimamia Palestina, serikali ya Uingereza sasa imeamua kumsaidia mvamizi na mhalifu badala ya wahanga."

Naftali Bennett na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson

Uamuzi huu wa serikali ya Uingereza umeonesha tena uongo wa madai ya nchi hiyo eti wa kuunga mkono na kutetea haki za binadamu za mataifa mbalimbali yanayokandamizwa hasa ikitiliwa maana kwamba, siku hiyo hiyo ya Ijumaa makumi ya raia wa Palestina walipigwa risasi na kujeruhiwa na askari wa Israel wakifanya maandamano ya amani huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kushadidi kwa jinai na uhalifu wa Israel huko Palestina ni kieleelzo cha kiwango cha wahka na wasiwasi wa Wzayuni na kunafanyika kwa lengo la kuwatia woga Wapalestina. Hata hivyo wameghafilika kwamba, raia wa Palestina, wakiwemo wa Ukingo wa Magharibi, wamefikia natija kwamba, mapambano ndiyo njia pekee ya kujikomboa kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu na wabaguzi. Kwa msingi huo na kutokana na kushindwa mara kwa mara, utawala wa Kizayuni umeamua kukimbilia msaada wa madola ya kigeni kwa ajili ya kuzibana zaidi harakati za mapambano ya ukombozi huko Palestiina.

Ni katika mazingira hayo ndipo Uingereza ilipochukua uamuzi wa kuitangaza harakatia ya mapambano na ukombozi wa Palestina ya Hamas kuwa ni kundi la kigaidi ili katika upande mwingine iunge mkono mwenendo wa baadhi ya nchi saliti za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel.