Nov 21, 2021 10:08 UTC
  • Huduma mpya ya London kwa Tel Aviv kwa kuituhumu Hamas kuwa ni kundi la kigaidi

Katika kuendeleza siasa zake dhidi ya taifa la Palestina na kuunga mkono utawala haramu wa Israel, Uingereza imetuhumu na kuitangaza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Paletina Hamas kuwa ni kundi la kigaidi.

Ijumaa iliyopita Priti Patel, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza wa Chama cha Wahafidhina alitoa taarifa na kupiga marufuku shughuli za harakati hiyo nchini humo. Huku akikariri tuhuma zisizothibitishwa dhidi ya Hamas, Patel alisema: 'Hamas ina uwezo mkubwa wa kigaidi zikiwemo silaha nyingi za kisasa na vilevile suhula za mafunzo ya ugaidi na ndio maana leo nimeamua kupiga marufuku shughuli zake hapa nchini.'

Mara tu baada ya kutangazwa marufuku hiyo, Naftali Bennett, Waziri Mkuu na Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel waliandika katika kurasa zao za Twitter wakifu na kushukuru hatua hiyo ya Uingereza dhidi ya Hamas.

Serikali ya kihafidhina ya Uingereza inahesabiwa kuwa moja ya waungaji mkono wakubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na licha ya kuendelea jinai za utawala huo wa kigaidi dhidi ya watu wa Palestina lakini haijawahi kubadilisha msimamo wake kuhusu uungaji mkono huo kwa Wazayuni watenda jinai. Kama tulivyoshuhudia karibuni, serikali ya London haikuchukua hatua yoyote ya kulaani mauaji ya kinyama yaliyotekelezwa karibuni na utawala wa Tel Aviv katika vita vyake vya kichokozi dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, bali ingali inauuzia utawala huo silaha ambazo unazitumia kutekeleza jinai dhidi ya Wapalestina wasi ona hatia. Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza mwezi Septemba uliopita alifumbia macho mashambulio ya kinyama yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kutangaza wazi kuwa London itadhamini usalama wa Israel kwa gharama na njia yoyote ile.

Priti Patel

Kutangazwa Hamas na serikali ya kihafidhina ya Uingereza kuwa ni kundi la kigaidi kunapelekea kuulizwa swali hili kwamba je, kundi hilo la mapambano ya ukombozi wa Palestina limeshawahi kutekeleza kitendo chochote cha ugaidi dhidi ya Uingereza au nchi yoyote ya Ulaya au hata kuchukuliwa kuwa ni tishio dhidi ya nchi hizo?

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza amehalalisha kitendo chake hicho dhidi ya Hamas kwa kuashiria uwezo wake wa kijeshi katika hali ambayo uwezo huo wa Hamas ni kwa ajili tu ya kukabiliana na hujuma za kikatili na kigaidi za utawala wa kibaguzi wa Israel, kama ile iliyotekelezwa kwa muda wa siku 12 katika Ukanda wa Gaza Mei mwaka huu ambapo mamia ya Wapalestina wasio na hatia waliuawa shahidi na kujeruhiwa. Hujuma hiyo ilikuwa kubwa na ya kinyama kiasi kwamba hata waungaji mkono wa Magharibi wa utawala huo wa Kizayuni walilazimika kuilaani hata kama ni kwa maneno matupu tu.

Nukta nyingine muhimu katika uwanja huo ni kwamba licha ya London kuchukua msimamo wa kinafiki kuhusiana na suala zima la ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zilizoghusubiwa na Wazayuni mwaka 1967, au kulaani kidhahiri tu baadhi ya unyama unaofanywa na utawala wa Tel Aviv dhidi ya Wapalestina lakini ni wazi kuwa Uingereza bado ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa utawala huo katika ngazi za kimataifa.

Mashambulio ya kikatili ya Israel katika Ukanda wa Gaza

Uingereza si tu inaupa utawala haramu wa Israel misaada mbalimbali ya kifedha, kiuchumi na silaha za kisasa bali imekuwa ikiunga mkono hatua tofauti za kigaidi na kijeshi za utawala huo dhidi ya Wapalestina yakiwemo mashambulizi ya 2008, 2012 na 2014. Katika hujuma ya Mei mwaka huu pia Uingereza iliutetea vikali utawala huo wa kigaidi na kuyatuhumu makundi ya Palestina kuwa ndiyo yalisababisha vita hivyo. Ushaihidi uliopo unaonyesha kuwa utawala ghasibu wa Israel umekuwa ukitumia silaha unazopewa na Uingereza kukandamiza na kuua kwa umati raia wa Palestina wasio na hatia na hasa wanawake na watoto wadogo.

Katika uwanja huo, Andrew Smith, mwanachama wa kampeni ya kukabiliana na mauzo ya silaha za Uingereza kwa utawala wa Israel anasema: Ushahidi unaonyesha kwamba serikali ya Uingereza inatekeleza mambo kinyume na matamshi inayotoa na hilo linathibitisha wazi undumakuwili na unafiki ulioko katika siasa zake za nje.

Tags