Nov 23, 2021 08:11 UTC
  • Kuendelea ubaguzi wa rangi Marekani

Uamuzi wa mahakama ya Marekani wa kufutilia mbali mashtaka ya mauaji yaliyokuwa yanamkabili kijana mmoja mweupe aliyehusika na mauaji ya watu wawili katika maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo mwaka uliopita, kwa mara nyingine umeamsha hasira ya wengi katika nchi hiyo ya Magharibi.

Mahakama ilimuondolea kijana huyo kwa jina Kyle Rittenhouse, makosa yote ya mauaji ya watu wawili, kumjeruhi wa tatu, kuhatarisha usalama wa waandamanaji kwa kuwasha moto, uasi na wizi wa tarehe 25 Agosti 2020 katika eneo la Kenosha katika jimbo la Wisconsin.

Uamuzi huo wa mahakama umeibua utata mwingine nchini Marekani kuhusiana na suala zima la ubaguzi wa rangi na ubebaji silaha usiodhibitiwa. Uamuzi huo ulikuwa wa kibaguzi, kidhalimu na wa upendeleo moja kwa moja kadiri kwamba hata Rittenhouse mwenyewe hakuamini masikio yake ulipotangazwa na mara tu baada ya kutangazwa alishindwa kujidhibiti kwa furaha baada ya mahakama kutoa hukumu isiyotarajiwa kwa manufaa yake. La kuchekesha ni kwamba katika kujitetea Rittenhouse alidai kuwa alitekeleza mauaji hayo kwa ajili ya kulinda usalama wake. Katika upande wa pili, umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika nje ya mahakama waliandamana dhidi ya hukumu hiyo huku wakiwa wamebeba mabango yaliyolaani uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo.

Kyle Rittenhouse

Kijana huyo mweupe muuaji amebadilika na kuwa shujaa mkubwa kati ya magenge ya ubaguzi wa rangi Marekani na hata Donald Trump, rais wa zamani wa nchi hiyo amemsifu kwa ukatili wake huo. Hakika hukumu ya mahakama hiyo ya Marekani inathibitisha wazi muendelezo wa ubaguzi wa rangi na undumakuwili unaotekelezwa dhidi ya jamii ya weusi na jamii nyinginezo za wachache katika nchi hiyo inayodai kuwa kinara wa kupigania haki na uhuru duniani.

Uzoefu wa miaka ya nyuma unaonyesha kwamba mtu mweusi anapohusika na hatia kama hiyo, vyombo vya mahakama vya nchi hiyo hukabiliana naye kwa mabavu na kwa njia isiyo ya kiutu. Jambo hilo limeamsha hasira na malalamiko ya tasisi na jumuiya za weusi wa nchi hiyo. Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International pia limetoa taarifa likisema: "Ukweli mchungu unaonyesha kwamba mahakama  na jamii ya Marekani imejengeka katika  msingi wa ubora wa watu weupe na ubaguzi dhidi ya weusi."

Kufuatia uamuzi huo wa kidhalimu wa mahakama ya Marekani uliopelekea kuachiliwa huru  Mmarekani mweupe mbaguzi wa rangi na muuaji aliyeua watu wawili bila kujali lolote na pia aliye na rekodi ndefu ya uhalifu, sasa kuna uwezekano kuwa nchi hiyo kwa mara nyingine itashuhudia maandamano na makabiliano kati ya wabaguzi wa rangi wanaounga mkono ubebaji silaha na jamii ya weusi na hata wahamiaji kutoka nchi za Amerika ya Latini. Weusi na wahamiaji hao wanaamini kuwa vyombo vya mahakama vya Marekani vimejengeka katika msingi wa ubaguzi wa rangi dhidi ya jamii za weusi na wahamiaji na bila shaka kesi ya Rittenhouse ni thibitisho la wazi katika uwanja huo.

Katika miaka ya karibuni na hasa katika utawala wa Donald Trump, kwa kutilia maanani mitazamo yake ya mrengo wa kulia na ya kibaguzi, ubaguzi wa rangi umeenea sana Marekani. Trump ni mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa magenge ya ubaguzi wa rangi yanayoamini kwamba watu weupe ni bora kuliko weusi na ambaye mara nyingi alitetea wazi wazi harakati hizo za kibaguzi dhidi ya jumuiya na taasisi za kutetea haki za watu weusi.

Maelfu waandamana Marekani kupinga hukumu iliyotolewa kwa manufaa ya Kyle Rittenhouse

Ubaguzi wa rangi ni suala ambalo huzusha mjadala mkali katika jamii ya Marekani. Alireza Rezakhah, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Ubaguzi wa rangi ni suala lililokita mizizi, la kihistoria na hata sehemu ya utamaduni wa Marekani. Fikra za Kimarekani kimsingi zinachochea na kuhamasisha ubaguzi wa rangi dhidi ya jamii za weusi na wachache na kuwachukulia kuwa raia wa daraja la pili. Katika mazingira ya sasa ambapo magenge ya ubaguzi wa rangi yanaendelea kuimarika katika nchi za Magharibi na hasa Marekani, ni wazi kuwa jamii za weusi na wahamiaji kutoka nchi za Amerika ya Latini zinakabiliwa na hatari kubwa ya siasa za mabavu na ubaguzi wa magenge hayo yanayoungwa mkono na vyombo vya dola.

Tags