Nov 24, 2021 12:18 UTC
  • Mashauriano ya Grossi Tehran; Iran yadhamiria kufuatilia miradi yake ya nyuklia

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambaye juzi alifanya ziara hapa Tehran jana Jumanne alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran kuhusu kuendeleza ushirikiano kati ya pande mbili.

Muhammad Eslami Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran baada ya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alisisitiza namna Iran ilivyodhamiria kutekeleza miradi yake ya nyuklia na kueleza kuwa: Katika mazungumzo hayo Rafael Grossi amebainisha mara kadhaa kwamba hakuna ukengeukaji wowote katika miradi ya nyuklia ya Iran na kwamba Iran inatekeleza shughuli zake za nyuklia kwa mujibu wa makubaliano na kanuni zilizowekwa.  

Muhammad Eslami, Mkuu wa Shirika Atomiki la Iran 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) pia ameeleza kuwa: Tunataka kuendeleza kazi na ushirikiano wa pande mbili ili kufikia nyanja za pamoja. 

Rafael Grossi amefanya ziara hapa Tehran katika kukaribia kikao cha Bodi ya Magavana ya IAEA kilichopangwa kufanyika  Jumatano wiki hii. Kuhusiana na suala hilo tovuti ya  Axius News imeripoti kuwa sasa nchi za Magharibi ziko chini ya mashinikizo katika kikao cha Bodi ya Magavana ili kuweza kuikosoa Iran. Hii ni katika hali ambayo Iran imekuwa ikiushauri wakala wa IAEA kusalia katika mkondo wa ushirikiano wa kiufundi na kutoziruhusu baadhi ya nchi  kufanikisha malengo yao ya kisiasa kwa jina la IAEA.

Iran aidha iliendelea kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA kwa muda wa miezi 15 baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika mapatano hayo ya nyuklia mwaka 2018; na kisha ikaanza taratibu kupunguza ahadi na uwajibikaji wake katika mapatano hayo kufuatia pande za Ulaya kushindwa kutekeleza ahadi zao ikiwemo kuifungulia Iran njia za kifedha na kibenki huku serikali ya Marekani pia ikiendeleza vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, katika ziara za karibuni za Grossi hapa Tehran Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliafiki pia mara mbili mapatano ya kiufundi kwa lengo la kudhamini kuendelezwa usimamizi wa IAEA katika taasisi zake za nyuklia lakini Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo ameendelea kuwasilisha maombi kwa Iran yaliyo nje ya masuala hayo ya usimamizi.

Suala jingine muhimu lililoikasirisha Iran ni kutekelezwa hatua za uharibifu katika taasisi zake za nyuklia na kuuliwa kigaidi wasomi wa Iran na utawala wa Kizayuni ambapo hadi sasa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) haujaonyesha wala kutoa radiamali yoyote mkabala wa mashambulizi hayo. Hii ni katika hali ambayo kama alivyosema Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran; wakala wa IAEA unajua vyema kuwa utawala wa Kizayuni umefanya vitendo vya uharibifu na kigaidi katika ardhi ya Iran; vitendo ambavyo vimenyamaziwa kimya na kufumbiwa macho na baadhi ya nchi zinazodai kutetea haki za binadamu duniani. Hujuma na mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni yamesababisha pia athari kubwa katika baadhi ya masuala ya kiufundi. 

Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran 

Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; kadhia zinazoendelea kati ya Iran na IAEA zote zinahusiana na masuala ya kiufundi, na IAEA haipasi kuathiriwa na mashinikizo ya kisiasa na hitilafu za kiufundi yanayochochewa hasa na nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran. 

Kwa kuzingatia kukaribia wakati wa kuanza mazungumzo kati ya Iran na kundi la 4+1 huko Vienna, Austria; na pia kufanyika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki mazungumzo ya Jumanne wiki hii ya Rafael Grossi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran  na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran yanaweza kuwa fursa kwa ajili ya wakala huo na hasa kwa Rafael Grossi ili mara hii aweze kutoa ripoti iliyo mbali na dhamira za kisiasa na mashinikizo ya maadui wa Iran kuhusu miradi ya nyuklia ya nchi hii inayofanyika kwa  malengo ya amani.