Nov 24, 2021 15:08 UTC
  • Amnesty yaonya: Maafa ya kibinadamu yataikumba Afghanistan isipoondolewa vikwazo

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema, ikiwa Afghanistan haitaruhusiwa kutumia akiba zake za benki kwa ajili ya kusaidia watu wake, maafa ya kibinadamu yataikumba nchi hiyo katika kipindi cha miezi ijayo.

Amnesty imeeleza katika ripoti yake kwamba, kusimamishwa misaada ya nje, kuzuiliwa mali za serikali ya Afghanistan na vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa Taliban, vimeifanya nchi hiyo ambayo inataabishwa na kiwango cha juu cha umasikini ikumbwe na mgogoro kamili na hali mbaya ya kiuchumi ya pande zote.

Kwa mujibu wa ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA, watu milioni 22 na lakini nane wanakabiliwa na baa la njaa na ukosefu mkubwa wa chakula. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP nalo pia limeripoti kuwa, hivi sasa kuna watoto wasiopungua milioni moja wanaoteseka kwa lisheduni nchini Afghanistan.

Hayo yanaelezwa huku Umoja wa Mataifa wenyewe ukitangaza kuwa zinahitajika zaidi ya dola milioni 200 za misaada ya kibinadamu kwa mwezi ili kuepusha maafa ya kibinadamu nchini humo.

Wakati huohuo Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu ICRC, nalo pia limeungana na Amnesty International kusisitiza kuwa njia pekee ya kuivua Afghanistan na baa la njaa ni kuondolewa vikwazo vya kibenki ilivyoekewa nchi hiyo.

Mkuu wa operesheni za ICRC Dominic Steelhart amesema, vikwazo vya kiuchumi vimeshadidisha hali mbaya iliyonayo Afghanistan na akasisitiza kwamba kuondolewa vikwazo vya kibenki ndio njia pekee ya kuiepusha nchi hiyo na baa la njaa.

Hivi karibuni, Mwakilishi maalumu wa Rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan Zamir Kabulov alikosoa hatua iliyochukuliwa na Marekani kuzuia mali za Afghanistan na akasema: Marekani na Wamagharibi wana dhima kubwa zaidi kuhusiana na mgogoro na hali mbaya ya sasa ya Afghanistan; kwani baada ya kushindwa wameondoka Afghanistan na kuzizuia mali za nchi hiyo kama njia ya kukomoa na kulipiza kisasi.../

Tags