Nov 25, 2021 14:39 UTC
  • Nusu ya wanawake duniani ni wahanga wa ukatili wa kijinsia; Afrika Kusini inaongoza

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, nusu ya wanawake duniani ni wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia vitendo ambavyo vinaripotiwa kuongezeka tangu lilipoibuka janga la virusi vya Corona duniani.

Ripoti hiyo imetolewa sambamba na kampeni ya kimataifa ya siku 16 dhidi ya ukatili wa kijinsia iliyoanza Alkhamisi ya leo Novemba 25 ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Ukatili Dhidi ya Wanawake.

Matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa yanaonyesha kuwa, kuanzia Aprili mwaka jana (2020) asilimia 45 ya wanawake waliohojiwa wenye umri wa miaka 18 hadi 49 walidai kuwa, wamewahi kuwa wahanga wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na kwamba, kuna mtu mwanamke mwingine wanayemjua ambaye naye aamewahi kukumbwa na ukatili huo.

Afrika Kusini inatajwa kuwa nchi inayoongoza dunia kwa ukatili dhidi ya wanawake, jambo ambalo serikali ya nchi hiyo imeshindwa kulikomesha.

Kampeni ya kimataifa ya dhidi ya ukatili wa kijinsia 

 

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa iliyoangazia athari za janga la COVID-19 kwa usalama wa wanawake nyumbani na katika maeneo ya umma imeonesha kuwa hisia za usalama za wanawake zimepotea, na kusababisha athari mbaya kwa hali yao ya kiakili na kimihemko.

Mizozo, majanga ya kibinadamu na ongezeko la majanga yatokanayo na tabianchi yamesababisha viwango vya juu vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, hali ambayo imeshika kasi zaidi wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Katika kuadhimisha siku 16 za harakati za kupinga ukatIli dhidi ya wanawake  shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN Women linapaza sauti za manusura watatu wa ukatili.