Nov 26, 2021 02:47 UTC
  • Indhari ya UN kuhusiana na kushamiri ubaguzi na uenezaji chuki ndani ya jamii ya Marekani

Fernand de Varennes, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu za jamii za wachache, ametahadharisha juu ya kuzidi kupanuka ufa wa kukosekana usawa na uenezaji chuki dhidi ya jamii za wachache katika mfumo wa vyombo vya mahakama na vyombo vya habari vya Marekani na kutilia mkazo udharura wa kuanzishwa sheria ya kimataifa ya kukabiliana na uenezaji chuki.

De Varennes ameeleza hayo katika ripoti yake, baada ya safari ya siku 14 ya kuitembelea Marekani na akaongeza kwamba, watu wa jamii za wachache nchini humo wangali "wanataabika kwa ubaguzi, kukosekana usawa na mahubiri ya uenezaji chuki". Aidha amesema, hali mbaya ya kiafya iliyosababishwa na janga la dunia nzima la corona ambalo limesababisha pia hali mbaya ya kiuchumi, yote hayo yameshadidisha mkosekano huo wa usawa na kwamba jamii hizo za wachache zilizotengwa ndizo zilizozidi kuathirika.

Fernand de Varennes

Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa anaitakidi kuwa, mfumo wa vyombo vya mahakama na magereza wa Marekani, ambao umekithiri wahalifu na wafungwa raia weusi na wenye asili ya Kilatini, ambao hawaendani na mlingano wa idadi ya watu, unazidi kuipa nguvu dhana ya kwamba "matajiri wanasemehewa na mafukara ndio wanaoadhibiwa."

Tahadhari hiyo kubwa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu hali isiyo ya kawaida na hata iliyofikia kiwango cha kuwa ni maafa ya jamii za mbari za wachache; na kuendelea aina mbalimbali za ubaguzi nchini Marekani ukiwemo ubaguzi wa rangi vinadhihirisha kuwepo hali mbaya ya kijamii ndani ya nchi hiyo inayopigia upatu suala la haki za binadamu. Na hili ni jambo ambalo hata rais wake Joe Biden amelikiri pia. Biden ameandika katika mtandao wa twitter: "ukweli ni kwamba,ubaguzi wa rangi wa kimfumo umetanda kwenye hali zote za maisha ya Kimarekani". Kuungama Joe Biden juu ya kuwepo ubaguzi wa rangi wa kimfumo nchini Marekani na hasa hali isiyo ya kawaida na isiyo ya kibinadamu wanayokabiliana nayo Wamarekani weusi katika nchi inayojigamba kuwa kiranja na mwongozaji wa haki za binadamu duniani, kunaweka wazi ukweli mchungu wa hali ya jamii ya Marekani. Kusema kweli, ubaguzi wa rangi, wa kielimu, kiajira, kijamii; na vilevile ukatili na ukandamizaji dhidi ya watu weusi vimegeuzwa kuwa jambo la kawaida nchini humo. Hivi sasa mwenendo huo unaendelezwa dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kilatini.

Katika miaka ya karibuni, hasa wakati wa urais wa Donald Trump, na kwa kutilia maanani mitazamo ya kibaguzi ya mrengo wa kulia anayofuata mwanasiasa huyo, ubaguzi wa rangi na ukatili na ukandamizaji wa kimbari vimeshamiri ndani ya jamii ya Marekani. Trump alikuwa mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa magenge ya Wamarekani weupe na wazungu wanaojiona bora, kiasi kwamba alisikika mara kadhaa akikosoa mavuguvugu ya kupinga ubaguzi wa rangi likiwemo lile la "Black Lives Matter" yaani "Maisha ya Weusi ni Muhimu." Donald Trump alikuwa rais pekee wa Marekani katika karne hii, ambaye alikataa waziwazi na hadharani kukemea ubaguzi wa rangi. Sambamba na hali hiyo, makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka ya mrengo wa kulia na wazungu wanaojiona bora, yamekuwa na nafasi kubwa zaidi katika siasa za ndani za Marekani; na makundi hayo yameshadidisha vitendo vya ukatili na ukandamizaji dhidi ya jamii za wachache kwa rangi na asili, wakiwemo Wamarekani weusi na wa Kilatini. Makundi hayo ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu ada, ambayo ubaguzi wa rangi ndio ajenda yao kuu, yanataka jamii zote za wachache zifukuzwe nchini humo.

Kimsingi hasa ni kwamba, ubaguzi wa rangi daima limekuwa likitajwa kama suala muhimu ndani ya jamii ya Marekani. Suala hili lina hali na pande tofauti, ambapo kwa hapa tunaweza kuashiria ubaguzi wa kielimu, wa kiajira na kijamii, ukatili na ukandamizaji dhidi ya jamii za mbari za walio wachache na hasa Wamarekani Weusi pamoja na miamala ya kiundumakuwili kuhusiana na Wazungu na jamii za wachache katika mfumo wa vyombo vya mahakama wa nchi hiyo.

Trump

Thamana Akwan, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "ubaguzi wa rangi nchini Marekani ni wa kimuundo na kimfumo; wakati mtu kama Trump anapotoa kaulimbiu za ubaguzi wa rangi anapata waungaji mkono na kuweza kukalia kiti cha urais, hali hiyo inaonyesha kuwa imani ya Wamarekani weupe kujiona bora haiwezi kutoweka kirahisi kwa sababu baadhi ya watu ndani ya nchi hiyo hawawezi kuwakubali watu Weusi abadani.

Ukweli ni kwamba fikra iliyotawala ndani ya Marekani ni ya ubaguzi wa rangi wa wazi na wa kificho na kuwadunisha raia Weusi na wenye asili ya Kilatini kwa kuwachukulia kuwa ni raia wa daraja la pili. Katika kipindi cha hivi sasa ambapo magenge na mirengo ya wazungu wanaojiona bora inazidi kuongezeka kila uchao katika nchi za Magharibi na hasa Marekani, raia weusi na wenye asili ya Latini wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kuandamwa na vitendo vya kikatili na vya ubaguzi wa rangi.../ 

 

Tags