Nov 26, 2021 02:48 UTC
  • Uingereza na Ufaransa zashambuliana kwa maneno kuhusu wakimbizi

Nchi mbili za Ulaya za Uingereza na Ufaransa zimeingia kwenye malumbano na vita vikali vya maneno baada ya wakimbizi 34 kupoteza maisha baharini wakati walipokuwa njiani kukimbilia Uingereza.

Ripoti ya gazeti la The Guardian imesema kuwa, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amezungumza kwa simu na waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson na kusema kuwa jukumu la kushughulikia wakimbizi linazihusu nchi hizo zote mbili. Vile vile aliitahadharisha Uingereza isitumie suala hilo kwa malengo ya kisiasa.

Kwa upande wake, waziri mkuu wa Uingereza aliilaumu Ufaransa kuhusu suala hilo na kusema, polisi wa Ufaransa walizembea kuchukua hatua za kulinda usalama wa wakimbizi hao. Boris Johnson alisisitiza kuwa, nchi mbili za Ufaransa na Uingereza zinapaswa kushirikiana katika upigaji doria kwenye mpaka wa majini wa nchi mbili lakini wakati huo huo akasema kuwa, vifo vya wakimbizi 34 waliokufa maji karibu na mpaka wa majini wa Ufaransa vinaonesha kuwa juhudi za viongozi wa Paris za kuendesha doria kwenye eneo hilo hazikuwa za kiwango cha kutosha.

La Manche (English Channel),  mpaka wa majini wa Uingereza na Ufaransa

 

Waziri Mkuu wa Uingereza amekwenda mbali zaidi na kusema, Uingereza imetatizika kutokana na kushindwa kuwakinaisha baadhi ya washirika wake hasa Ufaransa kushirikiana na London katika masuala hayo na ndio maana mambo hayatendeki inavyopasa kutendwa.

Hata hivyo Paris inapinga mwito wa Uingereza wa kutumwa askari zaidi wa Ufaransa kwa ajili ya kupiga doria katika mpaka wa majini wa nchi hizo mbili ikisema kuwa ina wasiwasi na madhara yatakayolikumba suala zima la haki ya Ufaransa ya kujiamulia na kujipangia yenyewe mambo yake.

Tags