Nov 26, 2021 10:08 UTC
  • Marekani yatakiwa kufutilia mbali vikwazo dhidi ya Iran na kutoingiza siasa katika mapatano ya JCPOA

Mkuu wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ameitaka Washington kufutilia mbali vikwazo vyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia kutoa dhamana kwamba serikali za baadaye za Marekani hazitakiuka na kupuuza mapatano ya kimataifa ya nyuklia yaliyofikiwa mwaka 2015 kati ya Iran na madola mengine makubwa duniani.

Ali Baqeri-Kani, aliyasema hayo jana Alkhamisi katika mahojiana na gazeti la Uingereza la The Independent.

Marekani ilijitoa katika mapatano hayo mwaka 2018 katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump na kisha kurejesha vikwazo dhidi ya Iran ambavyo awali vilikuwa vimefutiliwa mbali kufuatia mapatano hayo. Si hayo tu bali alianzisha kampeni kubwa ya kimataifa ya kuzilazimisha nchi nyingine huru duniani pia zifuate mkondo wake huo wa kutekeleza vikwazo hivyo haramu vya kiuchumi dhidi ya Iran.

Licha ya Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden kukiri kwamba vikwazo hivyo havijakuwa na taathira yoyote ya maana kwa Iran na kutangaza utayari wa serikali yake kurejea katika meza ya mazunguzo ya JCPOA lakini pamoja na hayo hajachukua hatua yoyote ya kufutilia mbali vikwazo hivyo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran.

Ali Baqeri-Kani

Kufikia sasa duru sita za mazungumzo zimefanyika mjini Vienna Austria kuona iwapo serikali ya Biden itatekeleza ahadi zake kuhusiana na mapatano ya JCPOA au la. Kikao cha saba kimepangwa kufanyika mjini humo mwishoni mwa mwezi huu.

Afisa huyo wa Iran ametahadharisha kuwa mazungumzo hayo pia yatafeli kufikia malengo yanayokusudiwa iwapo Marekani haitachukua uamuzi wa kuondoa vikwazo na kutoa dhamana ya kutoingizwa siasa katika mapatano ya JCPOA.