Nov 27, 2021 04:37 UTC
  • Rais Lukashenko: Marekani inataka kuanzisha vita Belarus

Rais Alexander Lukashenko wa Belarus amesema Marekani inatumia mgogoro wa wakimbizi kutaka kuibua makabiliano baina ya nchi mbili hizo.

Rais Lukashenko amesema Washington imeazimia kuanzisha vita nchini Belarus kwa kuyatumia mataifa ya Poland, Ukraine na nchi za eneo la Baltic.

Rais wa Belarus ameeleza bayana kuwa, nchi za Ulaya hazitaki vita Belarus, lakini Marekani inafanya juu chini kuona nchi hiyo inatumbukia katika mgogoro na mapigano.

Amebainisha kuwa, "Marekani itasimama na kusambaza silaha ili tuuane wenyewe kwa wenyewe na uchumi wetu usambaratike. Kisha watarejea na dola ambazo zinachapishwa hivi sasa, eti kutusaidia." 

Marais wa Russia na Belarus

Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Ulaya pia unatumia pia siasa za kindumilakuwili na vikwazo kama inavyofanya Marekani kuishinikiza Belarus.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, lengo la nchi za Magharibi ni kumng'oa madarakani Rais Alexander Lukashenko wa nchi hiyo ya Ulaya Mashariki, ili kupandikiza mtu mwenye mielekeo ya Kimagharibi na adui wa Russia. 

Tags