Nov 27, 2021 12:32 UTC
  • Russia na China: Demokrasia ya Kimarekani itashadidisha makabiliano ya kiidiolojia

Mabalozi wa Russia na China nchini Marekani wamesema, kufanyika kongamano la demokrasia nchini humo kutashadidisha makabiliano ya kiidiolojia duniani.

Anatoly Antonov na Qin Gang, mabalozi wa Russia na China mjini Washington wametoa indhari hiyo katika makala ya pamoja iliyochapishwa na jarida la National Interest  na kueleza kwamba kuitishwa kongamano la demokrasia na Marekani kutasababisha kujitokeza nyufa za utengano duniani.

Katika makala yao hiyo, wanadiplomasia hao wa Moscow na Beijing wamesema, kongamano hilo la demokrasia ni matunda ya fikra za enzi za Vita Baridi ambazo haziendani na mtazamo wa kuelekea kwenye ustawi na maendeleo duniani.

Mabalozi wa Russia na China mjini Washington wametamka bayana kuwa, muelekeo huo wa kuitisha kongamano la demokrasia Marekani hautaweza kuzuia kujengeka muundo wa dunia ya kambi kadhaa, isipokuwa utaweza kupunguza tu kas ya mchakato wa uhakika huo.

Antonov na Gang wamesisitiza kuwa, muundo wa mahusiano ya kimataifa inapasa ujengeke juu ya msingi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na si kujengwa kwa kufuata usuli na mfumo ulioainishwa na baadhi ya nchi tu.

Marekani imeitisha kongamano la demokrasia litakalofanyika kwa njia ya mawasiliano ya video kuanzia tarehe 9 hadi 10 za mwezi ujao wa Desemba.

Viongozi wa nchi, wanaharakati wa haki za binadamu na wafanyabiashara kutoka nchi 110 duniani wamealikwa kushiriki katika kongamano hilo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, Hungary, China, Uturuki, Saudi Arabia, nchi zingine za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, Korea Kaskazini, Venezuela, Nicaragua, Sudan, Ethiopia na nchi nyingine kadhaa za Afrika, Amerika ya Latinin na Asia hazimo kwenye orodha ya waalikwa wa kongamano hilo.

Harakati hiyo ya kimaonyesho inafanyika huku taasisi zenye itibari kimataifa zikitilia shaka demokrasia ya Kimarekani kutokana na ukandamizaji wa kiraia, ubaguzi wa rangi na tukio la fedheha lililotokea nchini humo Januari 6, 2020 wakati wazungu wanaojiona bora waliposhambulia na kuvamia jengo la bunge la nchi hiyo.../

Tags