Nov 27, 2021 14:58 UTC
  • Maafa ya vifo vya wakimbizi katika mfereji wa Manch, matokeo ya mzozo kati ya Ufaransa na Uingereza

Zaidi ya wakimbizi 27 kutoka pwani ya kaskazini ya Ufaransa waliovuka Mfereji wa Manchi wakijaribu kufika katika ardhi ya Uingereza walighariki na kufariki Jumatano jioni, Novemba 24, baada ya boti yao kuzama.

Boti iliyokuwa imewabeba wakimbizi hao ambao wengi wao walikuwa Wakurdi, ilipinduka na kuzama katika Mfereji wa Manch baada ya kuondoka katika pwani ya Dunkirk kaskazini mwa Ufaransa.

Katika kukabiliana na mkasa huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliahidi kuwa Paris itawasaka na kuwatia nguvuni wasafirishaji haramu wa binadamu waliosababisha maafa  hayo. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, pia alitoa wito wa kufanyika mkutano wa haraka wa Baraza la Mawaziri kujadili suala hilo na kuchukua uamuzi juu ya mgogoro huo.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa 

Licha ya msimamo huo wa Paris na London kuhusu maafa hayo ya wakimbizi, ukweli ni kwamba mkasa huu ni matokeo ya makabiliano na mizozo iliyopo kati ya serikali za Ufaransa na Uingereza na kutojali kwao kabisa hatima ya wahajiri katika safari hatari sana ya kutoka kaskazini mwa Ufaransa wakielekea kusini mwa Uingereza kupitia Mfereji wa Manch. Hivyo, kuwarushia tuhuma wasafirishaji haramu wa binadamu kunalenga kuficha wajibu na majukumu ya serikali za Ufaransa na Uingereza katika maafa hayo. Takriban watu 26,000 wamewasili pwani ya Uingereza kupitia Mfereji wa Manch kwa kutumia boti ndogo tangu mwanzoni mwa 2021, idadi ambayo imeongezeka mara tatu ilikinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. 

Mfereji wa Manch ulioko baina ya Ufaransa na Uingereza ni mojawapo ya njia za majini zenye shughuli na harakati nyingi zaidi duniani na ni hatari sana kuvuka eneo hilo kwa boti ndogo, hasa katika misimu ya vuli na masika na siku zenye mawimbi na dhoruba kali. Njia hiyo ya majini na matukio yanayoambatana na majaribio ya wakimbizi kuelekea pwani ya Uingereza kupitia njia hii ya maji daima imekuwa ikizusha mizozo na mivutano kati ya Paris na London. Maafisa wa serikali ya kihafidhina ya Uingereza wanasema juhudi za Ufaransa za kudhibiti mzozo huo hazitoshi. Wakati huo huo, maafisa wa Paris wameikosoa London kwa kutotekeleza ahadi yake ya msaada wa kifedha kwa Ufaransa ili kuzuia wimbi la wahajiri wanaotaka kuvuka Mfereji wa Manch kuelekea Uingereza. Suala lenye umuhimu mkubwa zaidi kwa sasa ni kwamba, waathiriwa wa mizozo na mivutano ya Ufaransa na Uingereza, ambayo inahusu masuala kadhaa kuanzia haki za uvuvi hadi kadhia ya udhibiti wa wahajiri, ni wahamiaji wanaoingia katika safari ngumu sana na hata kughariki baharini wakitokea Asia Magharibi hadi Ulaya.

Image Caption

 

Ufaransa, ambayo daima imekuwa na msimamo hasi kuhusiana na wahajiri wanaotafuta hifadhi, inatafuta njia kuwafukuzilia mbali wakimbizi hao na kujinasua na mgogoro huo. Licha ya kuwa na habari juu ya ongezeko la wahajiri katika pwani ya kaskazini mwa Ufaransa, hasa karibu na Mfereji wa Manch, Paris imekuwa ikionesha taa ya kijani kwa wahajiri hao kwa kufumbulia macho na kupuuza suala hilo. Uingereza, kwa upande mwingine, imekuwa ikifuata sera kali dhidi ya wahajiri na wakimbizi tangu ilipojitoa kwenye Umoja wa Ulaya, na imekataa katakata kuwapokea kupitia njia ya kupitisha sheria mpya zinazohusiana na wahajiri. Bella Sankey ambaye ni mkuu wa kundi la watetezi wa haki za wakimbizi wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza anasema: "Uingereza na Ufaransa hazina irada na azma ya kisiasa ya kutatua mzozo wa wahamiaji na wakimbizi katika Mfereji wa Manch. Vifo vya hivi majuzi vya wahamiaji katika mfereji huo vilitabirika na kulikuwepo uwezekano wa kuepukika. Kwa bahati mbaya, tuna serikali nchini Uingereza ambayo inaendeleza kikamilifu sera iliyoshindwa ya kuwafukuza watu wanaotafuta hifadhi nchini, bila kujali matokeo."

Ulaya ina rekodi mbaya kuhusiana na wahajiri wanaotafuta hifadhi na daima  imekuwa ikikabiliana nao kwa msimamo hasi na wakati mwingine kwa kutumia mabavu. Nchi za Ulaya zinafanya jitihada za kuzuia wahajiri kuingia barani huo na kuwarejesha makwao wale waliofanikiwa kuingia katika nch hizo kwa mashaka na tabu kubwa. Kwa sasa kuna idadi kubwa ya wahajiri wanaotafuta hifadhi ambao wanatangatanga katika hali mbaya kwenye nchi za Ulaya. Mizizi ya mgogoro wa wakimbizi hao pia iko katika sera za kindumakuwili na za kinafiki za nchi za Magharibi katika kupambana na ugaidi na umaskini.

Tags