Nov 28, 2021 11:59 UTC
  • Wanawake nchini Italia waandamana kulaani ukatili wa kijinsia

Mitaa na barabara za Rome, mji mkuu wa Italia zimeshuhudia maandamano makubwa ya wanawake wanaolalamikia ongezeko la kesi za ukatili wa kijinsia na mizozo ya kinyumbani.

Maelfu ya wanawake wamejitokeza kushiriki maandamano hayo ya kutaka kukomeshwa dhulma na ukatili dhidi yao, hususan katika ngazi za wanandoa na familia. Wametoa mwito wa kuundwa sheria kali za kukabiliana na dhulma za kijinsia dhidi yao, wakisisitiza kuwa tatizo hilo halipaswi kuendelea kupuuzwa.

Takwimu zinaonesha kuwa, wanawake milioni 7 wa Italia ni wahanga wa ukatili wa kijinsia kila mwaka, huku 120 miongoni mwao wakiuawa kutokana na ukatili huo kila mwaka.

Kwa mujibu wa polisi ya Italia, wanawake 109 wameshauawa hadi sasa kutoka na ukatili dhidi ya wanawake katika nchi hiyo ya Ulaya, tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

Wanawake wa Ufaransa waliandamana pia karibuni kulaani ukatili dhidi yao

Kesi za ukatili wa kijinsia hususan ukandamizaji na dhulma dhidi ya wanawake haswa katika ngazi ya familia zimeongezeka mno katika nchi za Ulaya.

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, nusu ya wanawake duniani ni wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, vitendo ambavyo vinaripotiwa kuongezeka tangu lilipoibuka janga la virusi vya Corona duniani.

Ripoti hiyo ilitolewa siku chache zilizopita, sambamba na kampeni ya kimataifa ya siku 16 dhidi ya ukatili wa kijinsia iliyoanza Alkhamisi ya Novemba 25 ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Ukatili Dhidi ya Wanawake.

Tags