Nov 29, 2021 02:39 UTC
  • Spishi mpya ya Omicron na ukosefu wa uadilifu katika kugawa chanjo za corona

Kugunduliwa spishi mpya ya kirusi cha corona nchini Afrika Kusini kinachojulikana kwa jina la Omicron na kuenea hadi barani Ulaya, kumezusha wasiwasi mkubwa wa kuambukizwa corona watu wengi zaidi duniani.

Lawama kubwa zinazotolewa hivi sasa zinaelekezwa kwa madola ya Magharibi ambayo yameshindwa kugawa kiuadilifu chanjo za corona au UVIKO-19 na zimeamua kuhodhi chanjo zote ili zisizifike kwa nchi maskini.

Hivi sasa dunia imekaribia kuingia kwenye wimbi jipya la ugonjwa wa corona katika hali ambayo nchi nyingi maskini na zilizo nyuma kimaendeleo zimeshindwa kugharamia zoezi la kuwapiga chanjo watu wao na hata kufuata maagizo ya watu wa afya ya kujikinga na maambukizi ya corona. Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kimesema, hadi hivi sasa nusu ya nchi za Afrika zimepiga chanjo kwa asilimia mbili tu, bali chini ya hapo.

Ukosefu huo mkubwa wa uadilifu katika kugawa chanjo za corona unashuhudiwa katika hali ambayo tangu mwanzoni mwa kuenea ugonjwa wa UVIKO-19 na kutangazwa kuwa hilo ni janga la dunia nzima, nchi tajiri ziliahidi kutofanya ubaguzi katika utoaji chanjo. Lakini mara baada ya kupatikana chanjo, nchi hizo zilisahau kabisa ahadi zao na kuligeuza suala hilo kuwa wenzo wa mashinikizo ya kisiasa huku mashirika yanayotengeneza chanjo nayo yakiangalia tu manufaa yao binafsi ya kifedha na kutoshughulishwa hata kidogo na maadili ya kiutu na kibinadamu. Matokeo yake ni kuwa, hivi sasa nchi nyingi za Magharibi zimeshapiga chanjo kwa zaidi ya asilimia 80 huku nchi za Afrika ndio kwanza zinasuasua na nyingine hazijaweza hata kudhamini fedha za kugharamia chanjo hizo.

Hatua ya nchi za Magharibi ya kuhodhi chanjo na kutozipa maskini zimekuwa na madhara kwa dunia nzima

 

Takwimu zinaonesha kuwa, katika hali ambayo wananchi wa Marekani wanaunda robo tu ya watu wote ulimwenguni, serikali ya nchi hiyo imehodhi na kujilimbikizia robo nzima ya chanjo zote za corona duniani.

Hii ni katika hali ambayo taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, muda wote zinaonya kuhusu madhara makubwa ya kutogawanywa kiuadilifu chanjo za UVIKO-19 duniani. Hivi karibuni Umoja wa Mataifa uligusia changamoto kuu zinazolikabilia zoezi la kugawa chanjo za corona duniani na kusema kuwa, nchi za Magharibi zimehodhi chanjo hizo, kuna vizuizi katika usafirishaji wa chanjo hizo, hakuna miundombinu inayotakiwa katika baadhi ya maeneo na muhimu kuliko yote, hakujatengwa fedha zinazotakiwa za kuziwezesha nchi maskini kukabiliana na ugonjwa huo.

Huko nyuma Luis Enjuanes, mtaalamu wa kemia na virusi raia wa Uhispania aliwahi kulalamikia ukosefu mkubwa wa ugawaji wa chanjo za UVIKO-19 duniani na kusisitiza kuwa, uamuzi wa Marekani na nchi za Ulaya si wa busara hata kidogo kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuzuka spishi mpya za corona katika maeneo mengine duniani ambayo hayajapigwa chanjo.

Luis Enjuanes, mtaalamu wa kemia na virusi raia wa Uhispania

 

Hivi sasa kumezuka spishi mpya ya corona ambayo nchi za Magharibi zinasema ni hatari zaidi kuliko zote, na imeleta hofu kubwa duniani. Spishi mpya ya corona ijulikanayo kwa jina la Omicron imetajwa kuwa ni aina hatari zaidi ya kirusi cha corona kilichowahi kutokea duniani.

Naye Gordon Brown, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza amesema kuwa, kuzuka spishi mpya ya kirusi cha corona iitwayo Omicron huko Afrika Kusini ni matokeo ya kuhodhiwa chanjo za ugonjwa huo na baadhi ya madola hasa ya Magharibi na kunyimwa nchi maskini duniani.

Kirusi kimpya cha Omicron kimegunduliwa huko Afrika Kusini katika hali ambayo nchi za Afrika zina upungufu mkubwa wa vifaa vya tiba, misaada inayotolewa kutoka nchi wafadhili ni kidogo, na hata juhudi za nchi mbalimbali za Afrika za kujaribu kujidhaminia chanjo za kujikinga na UVIKO-19 zinakwamishwa na madola makubwa ambayo pia hayaziruhusu nchi nyingine zikiwemo za Afrika kuwa huru katika shughuli zao za maendeleo. Sasa hivi nchi za Ulaya na Marekani zinatumia chanjo ya corona kama wenzo wa kuendeleza ukoloni barani Afrika. Lakini sasa hivi wakoloni hao wamekumbana na kirusi ambacho hakichagui, bali nchi hizo hizo za kikoloni ndizo ambazo zimekuwa wahanga wakubwa wa ugonjwa wa corona.

Tags