Nov 29, 2021 12:02 UTC
  • Mazungumzo ya Vienna, changamoto na matarajio

Leo Novemba 29 mji mkuu wa Austria, Vienna ni mwenyeji wa mazungumzo baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Nchi za 4+1 ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya

Ali Baqeri, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa aliwasili Vienna Jumamosi akiongoza ujumbe wa  wataalamu wa masuala ya sheria, benki na nishati kwa ajili ya kushiriki katika mazungumzo hayo. Katika siku za hivi karibuni Baqeri amefanya mazungumzo na wajumbe wa Russia na China na pia afisa mwandamizi wa Umoja wa Ulaya, Enrique Mora, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Pamoja ya Mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Iran ina azma imara ya kufikia mapatano mazuri lakini misimamo inayokinzana ya Marekani ni moja kati ya changamoto kubwa katika mchakato wa mazungumzo. Pamoja na kuwa serikali ya Rais Joe Biden imetangaza hamu ya kurejea katika mapatano ya JCPOA lakini wakati huo huo inatumia lugha ya vitisho ili kuishinikiza Iran kisiasa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika duru hii ya mazungumzo haitaki tena kupoteza wakati na inataka matokeo yapatikane. Kwa kuzingatia misimamo inayolegelega ya Marekani, Iran inasisitiza kuthibitishiwa kivitendo kuwa upande wa pili katika mapatano ya JCPOA utatekeleza ahadi zake.

Kwa msingi huo, kufikiwa matokeo yanyaokubalika katika mazungumzo ya Vienna kutategemea nukta kadhaa.

Richard Bensel mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Cornell ameashirikia mchakato wa kuhuishwa mapatano ya JCPOA na kusema kuwa moja ya changamoto kubwa katika kupatikana mapatano ya kudumu baina ya Iran na Marekani ni hitilafu zilizoko katika mfumo wa Marekani. Anasema hitilafu hizo zinapelekea serikali ya Biden ishindwe kutoa dhamana kuwa itatekeleza ahadi inazotoa katika mapatano.

Uzoefu unaonyesha kuwa, mashinikizo yoyote dhidi ya Iran kwa lengo la kuilazimisha iafiki kuhuishwa mapatano ya JCPOA bila kudhaminiwa maslahi yake yatapelekea kukosekana muafaka. Malengo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna ni kuondolewa kikamilifu vikwazo vya Marekani kwa njia ambayo itaweza kuthibitishwa  sambamba na kuwezeshwa taifa la Iran kunufaika kisheria na teknolojia ya nyuklia.

Kwa kuzingatia hayo,  tunaweza kuashiria nukta mbili kuhusu mazungumzo ya Vienna.

Kwanza ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefika katika meza ya mazungumzo huko Vienna kwa mujibu wa haki yake ya kisheria katika fremu ya mapatano ya JPCO na kile inachotaka ni kuondolewa vikwazo vyote kwa njia ambayo itaweza kuthibitishwa kivitendo.

Nukata ya pili ni kuhusu tofauti za kimitazamo baina ya pande mbili katika mazungumzo. Tofauti hizi zinaweza kuathiri vibaya mchakato wa mazungumzo na hata kupelekea yavunjike.

Ali Bagheri, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika makala aliyoandika katika gazeti la kila siku la Uingereza la Financial Times amesisitiza ulazima wa pande zote katika mazungumzo kufungamana na vipengee vya mapatano ya JCPOA na kusema: "Nchi za Magharibi na hasa Marekani zinajaribu kufanya 'mazungumzo' kwa ajili ya kufanikisha malengo ya kuzuia au kuweka vizingiti katika mpango halali wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Hii ni katika hali ambayo mpango wa nyuklia wa Iran unatekelezwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Iran inasisitiza kuwa mazungumzo yanapaswa kuwa na lengo  halisi linalofuatiliwa na pande zote zifungamane na lengo hilo.

Ali Baqeri, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesisitiza kuwa, Iran iko tayari kujibu hatua yoyote ya nia njema ya pande zingine katika JCPOA  sambamba na kutoa jibu muafaka kwa mashinikizo yoyote ya kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Tarajio kuwa Iran itatekeleza ahadi zake zote katika JCPOA huku upande wa pili ukiwa hautekelezi ahadi zake ni tarajio lisilo la kimantiki. Kukaririwa matakwa yasiyo ya kimantiki katika mazungumzo ya Vienna hakutakuwa na taathira katika maamuzi ya Iran ya kulinda na kutetea haki zake za kisheria. 

Hivi sasa, kwa kuzingatia changamoto na matarajio, inasubiriwa kuona ni kiasi gani mazungumzo ya Vienna yanaweza kupelekea kufikiwa maamuzi ya kisiasa ambayo yatafuatiwa na kuondolewa kikamilifu vikwazo dhidi ya Iran.

 

Tags