Nov 30, 2021 04:35 UTC
  • WHO: Afrika Kusini na Botswana inabidi zipongezwe na sio kuadhibibiwa kwa kugundua kirusi cha Omicron

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema jana, dunia inabidi iwashukuru wanasayansi wa Afrika Kusini na Botswana kwa kugundua kirusi kipya cha corona aina ya Omicron na kuutahadharisha ulimwengu kuhusu hatari ya kirusi hicho na sio kuziadhibu nchi hizo.

Kabla ya hapo Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuwa limeeleza kuwa bado haijajulikana iwapo kiwango cha maambukizi ya kirusi kipya cha corona cha Omicron kitakuwa cha juu ikilinganishwa na spishi nyingine kama ile ya Delta au la. Hata hivyo idadi ya watu waliofanyiwa vipimo vya corona katika nchi kadhaa za kusini mwa Afrika kufuatia kugunduliwa kirusi kipya inaendelea kuongezeka. 

Kabla ya hapo pia, Afrika Kusini ililalamika kwa kusema, inahisi "inaadhibiwa" kwa kugundua spishi mpya ya kirusi cha corona aina ya Omicron kutokana na marufuku mbalimbali zilizowekwa zikiwemo za kuzuia wasafiri kutoka nchi za kusini mwa Afrika kuelekea mataifa mengine ya dunia.

Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus

 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ilieleza katika taarifa iliyotoa Jumamosi wiki hii kwamba, marufuku za safari za ndege zilizowekwa kufuatia kugunduliwa spishi hiyo ni sawa na kuiadhibu nchi hiyo kwa sababu ya uwezo wake wa juu katika utaalamu wa kijenetiki na kuweza kugundua haraka spishi mpya.

Jana Jumatatu Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alizilaumu nchi zilizochukua sheria kali dhidi ya nchi za kusini mwa Afrika na kuongeza kuwa, hatua ya wanasayansi wa nchi mbili za Afrika Kusini na Botswana ya kuitahadharisha dunia kuhusu kirusi kipya cha corona inastahiki kupongezwa na kushukuriwa, na si kuziadhibu nchi hizo.