Dec 01, 2021 02:40 UTC
  • Kuunga mkono kundi la 4+1 kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Sambamba na kuanza duru ya saba ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 4+1 huko Vienna Austria, kumeongezeka himaya na uungaji kwa takwa la haki na la kisheria la Iran la kuondolewa vikwazo vya upande mmoja ilivyowekewa kidhalimu na Marekani.

Msimamo wa karibuni kabisa katika uwanja huo ni ule uliotangazwa na Mikhail Ulyanov, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna. Ulyanov amesema, msimamo wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna ni kuondolewa vikwazo vyote dhidi ya JCPOA na kwamba, Russia inayaona na kuyatambua matakwa ya Iran kuwa ni ya kisheria.

China nayo, mwanachama mwingine wa kundi la 4+1 imechukua msimamo unaoshabihiana na wa Russia.  Wang Wenbin, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China akizungumza siku ya Jumatatu, aliionyeshea kidole cha lawama Marekani na kuitaja kama ndiyo iliyozusha mgogoro katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kueleza kwamba, Washington inapaswa kufuta vikwazo vyote vya kidhalimu na vya upande mmoja dhidi ya Iran.

Msimamo mmoja wa China na Russia kuhusiana na udharura wa kuondolewa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran baada ya Washington kujitoa katika makubaliano hayo Mei 2018 na kuanza kuiandama Tehran kwa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ambayo yangali yanaendelea hadi sasa, inachukuliwa katika fremu ya kuunga mkono haki ya Iran katika uga huo.  

 

Umoja wa Ulaya nao na kundi la Troika ya Ulaya hazina chaguo jingine ghairi ya kkuyakubali matakwa ya Iran ambayo ni ya kisheria na kimantiki. Taarifa ya pamoja iliyotolewa na madola ya Ulaya katika kikao cha 65 cha Baraza Kuu la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Septemba mwaka huu (2021) sanjari na kukiri matokeo mabaya ya uamuzi wa upande mmoja wa kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ilieleza kuwa, kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran ni sehemu muhimu ya makubaliano hayo.

Iran imesisitiza bayana na kinaugaubaga tena siyo mara moja wala mara mbili kwamba, inachotaka ni kuondolewa vikwazo vyote vya kidhalimu vya Marekani dhidi yake na kwamba, hilo ndilo takwa kuu la Tehran katika mazungumzo ya mara hii ya Vienna Austria. Hili ni jambo lililotiliwa mkazo pia na Marais wa Ibrahim Raeisi wa Iran na Emmanuel Macron wa Ufaransa walipofanya mazungumzo yao kwa njia ya simu.

Kadhalika Iran inataka kupatiwa dhamana na hakikisho kutoka kwa serikali ya Marekani kwamba, haitajitoa tena katika makubaliano hayo na pia haitatumia vibaya nguvu iliyopo dhidi ya nchi wanachama wengine wa makubaliano hayo.

Fael Ibiatov, mhadhiri wa Chuo Kikuu nchini Russia anasema: Kwa kuzingatia kutokuwa na uhalali wa kisheria vikwazo vya Marekani dhidi ya Ira na ukweli huu kwamba, Tehran imetoa ushirikiano wa kiwango cha juu kabisa kuhusiana na kuweka wazi shughuli zake za miradi ya nyuklia, bila shaka umewadia wakati sasa wa taifa hili kuondolewa vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa taifa hili.

 

Hii ni katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni Marekani imeamua kuchukua mkondo wa kutoa vitisho na kudai kwamba, endapo mwenendo wa kupiga hatua miradi ya nyuklia ya Iran utaendelea, basi itashadidisha mashinikizo dhidi ya Tehran. Hata hivyo, Marekani inafahamu vyema kwamba, mbinu ya kuiwekea vikwazo Iran hakuna wakati ambao ilikuwa na natija bali itapelekea kutengwa zaidi Washington. Pengine ni kutokana na sababu hiyo ndio maana liicha ya kudaiwa kwamba, msimamo wa Washington kwa Tehran haujabadilika, lakini Jen Psaki msemaji wa Ikulu ya nchi hiyo White House amesema kuwa, njia bora ya kuamiliana na Iran ni mwenendo wa kidiplomasia.

Filihali kila kitu kiko wazi mbele ya macho ya kundi la 4+1 hususan Troika ya Ulaya kwa ajili ya kuyaokoa makubaliano hayo ya JCPOA. Kubakia makubaliano haya kunafungamana na kutekelezwa kivitendo takwa la Tehran ambalo ni la haki na la kisheria nalo ni kuondolewa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,

Endapo Washington itakwamisha mambo katika uga huu na kuja na matakwa yanayotaka kubadilishwa vipengee vya makubaliano hayo au kuja na matakwa ambayo kimsingi yapo nje ya makubaliano ya JCPOA katika mazungumzo ya sasa na wakati huo huo kupuuza matakwa ya kisheri ya Iran, hapana shaka kuwa, atayaebeba dhima ya matokeo mabaya ya kitendo ni upande wa pili yaani kundi la 4+1 pamoja na Marekani.

Tags