Dec 01, 2021 08:20 UTC
  • Uwezekano wa Umoja wa Mataifa kutowakubali wawakilishi wa Taliban na wanajeshi wa Myanmar

Wanadiplomasia wanasema kuna uwezekano mdogo mno wa kamati ya kuthibitisha nyaraka za utambulisho za wanadiplomasia wanaohudumu katika Umoja wa Mataifa kukubali nyaraka za utambulisho za wawakilishi wa kundi la Taliban linalotawala Afghanistan na wale wanaowakilisha wanajeshi wanaotawala Mynmar.

Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa ambao hawakutaka majina yao yatajwe wamesema ni jambo lililo mbali kwa kamati hiyo kuidhinisha majina ya wawakilishi wa watawala wa nchi mbili hizo katika kikao ambacho kimepangwa kufanyika leo Jumatano mjini New York ambayo ni makao makuu ya umoja huo ulio na wawakilishi wa nchi 193.

Inasemekana kuwa kitendo cha Umoja wa Mataifa kukubali wawakilishi wa Taliban au wanajeshi wa Myanmar kitakuwa na maana ya umoja huo kuwatambua rasmi watawala wa nchi hizo. Kamati iliyotajwa ya Umoja wa Mataifa iliyo na wanachama wa nchi 9 zikiwemo Russia, China na Marekani inatazamiwa kufanya kikao leo Jumatano kwa ajili ya kuchunguza itibari ya wanachama wote 193 wa Umoja huo.

Mtawala wa kijeshi wa Myanmar Min Aung Hlaing

Wajuzi wa masuala ya diplomasia wanasema wawakilishi wapya wa Afghanistan na Mynmar hawatakubaliwa wala kutambuliwa rasmi katika kikoa cha leo kwa kutilia maanani kuwa wanadiplomasia na mabalozi wa zamani wa nchi mbili hizo wangali wanahudumu katika nafasi zao katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.