Dec 01, 2021 11:01 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Kufungamana na Palestina; hatua ya kipropaganda ya Umoja wa Mataifa

Licha ya kupita miaka 44 tangu Umoja wa Mataifa utangaze tarehe 29 Novemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Kufungamana na Taifa la Palestina lakini hakuna lolote la maana ambalo limechukuliwa katika uwanja huo na badala yake hali ya Palestina inaendelea kuwa mbaya na ya kusikitisha mwaka hadi mwingine.

Tarehe 29 Novemba 1977 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa sauti moja kutengwa siku hiyo katika kalenda ya dunia kuwa siku ya kufungamana na watu wa Palestina na kuyataka mataifa yote wanachama wa umoja huo yaenzi na kuiheshimu siku hiyo. Licha ya kupita miaka 44 tokea kutangazwa rasmi siku hiyo lakini hali ya Wapalestina imeendelea kuwa mbaya na ya kusikitisha mwaka hadi mwaka.

Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds inayokaliwa kwa mabavu na wale wa Ukanda wa Gaza wanaishi chini ya mashinikizo makali ya mzingiro na vita vya walowezi wa utawala ghasibu wa Israel. Zahra Irshadi, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa anasema katika vita vya siku 12 vya Ukanda wa Gaza mwezi Mei uliopita, askari katili wa utawala wa Israel waliua kinyama Wapalestina 256 wakiwemo watoto 66 na wanawake 20, ambapo watu 13 walikuwa ni wa familia moja akiwemo mtoto mchanga wa miezi sita ambaye alizikwa katika kifusi cha nyumba yao iliyobomolewa na Wazayuni.

Maandamano ya kufungamana na Wapalestina mjini London

Ameongeza kuwa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa kufuatia mashambulizi hayo ya kinyama Wapalestina 3000 wakiwemo watoto 600 na wanawake 200 walijeruhiwa ambapo baadhi yao wamekuwa vimela maisha yao yote. Kwa mujibu wa tangazo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, tangu mwanzo wa Aprili mwaka uliopita wa 2020 hadi tarahe 31 Machi 2021 askari jeshi na usalama wa Israel waliua Wapalestina 21 wakiwemo wavulana 6 na kujeruhi wengine 1662 wakiwemo watoto 185 (7 wa kike na 178 wavulana) na wanawake 21.

Wakimbizi wa Kipalestina pia wanaendelea kuzuiwa kurejea katika ardhi zao za jadi ambapo wengi wanaishi katika nchi nyingine na katika kambi za wakimbizi. Sambamba na kuwadia mwaka wa 44 wa kutangazwa Siku ya Kimataifa ya Kufungamana na Palestina, wakimbizi wa Kipalestina wamefanya maandamano katika kambi za wakimbizi za al-Badawi na Nahrul Barid nchini Lebanon wakilaani jinai zinazotekelezwa na utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya Wapalestina na hasa wale wanaoshukiliwa mateka na utawala huo.

Licha ya utawala huo kutekeleza jinai kubwa dhidi ya Wapalestina wasio na hatia lakini madola ya Magharibi yanaendelea kuunga mkono kwa hali na mali dhidi ya maslahi ya Wapalestina. Katika hatua ya karibuni kabisa, serikali ya Uingereza na katika kukaribia Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Palestina, iliitangaza Harakati ya Mapambano ya Palestina Hamas kuwa kundi la kigaidi. Serikali ya Rais Joe Biden pia licha ya kuonyesha kidhahiri kuwa inakemea jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina lakini kama ilivyokuwa serikali ya kabla yake ya Donald Trump, imeendelea kuunga mkono utawala huo kwa hali na mali.

Mkusanyiko wa kufungamana na taifa la Palestina, Italia

Katika mazingira hayo, Umoja wa Mataifa kama ilivyokuwa katika kipindi chote cha miongo saba iliyopita, umekuwa ukinyamazia kimya jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina na hata mara nyingine kuziunga mkono moja kwa moja. Tatizo kubwa katika uwanja huo ni uungaji mkono unaotolewa na Marekani na washirika wake wa Magharibi na hasa Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel. Jambo la kusikitisha ni kuwa hata yale mashirika ya kimataifa ya Magharibi yanayodai kutetea haki za wanawake na watoto na kwa ujumla haki za binadamu, yamenyamaza kimya mbele ya jinai hizo za Wazayuni dhidi ya Wapalestina.

Tabia na siasa hizo za kimya za Umoja wa Mataifa mbele ya jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel zinaonyesha wazi kuwa Siku ya Kimataifa ya Kufungamana na Watu wa Palestina iliyotangazwa na umoja huo kwa hakika ni harakati ya kipropaganda na kimaonyesho tu ambayo inalenga kupunguza ukosoaji kuhusu kimya na uzembe wake katika kukabiliana na siasa za mabavu na ugaidi wa utawala wa Israel unaokiuka sheria za kimataifa kila uchao.

Tags