Dec 01, 2021 12:05 UTC
  • COVID-19 imesababisha kupungua kwa vifaa vya upimaji na utambuzi wa VVU

Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa za tiba kwa gharama nafuu, UNITAID, limesema usumbufu na ucheleweshaji wa huduma za kukabiliana na  Virusi vya Ukimwi (VVU) unaosababishwa na janga la COVID-19 ulisababisha kupungua kwa vifaa vya upimaji na utambuzi wa VVU kwa kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kuonekana ndani ya miongo miwili.

Katika taarifa ambayo imetolewa kwa mnasaba wa siku ya UKIMWI Duniani ambayo inaadhimishwa leo Desemba 1, msemaji wa UNITAID Hervé Verhoosel, anasema baada ya janga la COVID-19 hali imebadilika na vipimo hivyo vimepungua sana ikilinganishwa na miongo miwili iliyopita.

"UNITAID inatoa wito kwa wafadhili kuongeza ufadhili wa haraka kwenye vifaa vya upimaji wa Virusi Vya Ukimwi VVU ili kulinda maendeleo yaliyodhoofishwa na COVID-19 na njia salama ya kuzuia VVU kwa mamilioni ya watu ulimwenguni,” imeongeza.
Takwimu zilizokusanywa kwa pamoja na UNITAID na WHO zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2015 na 2020, idadi ya nchi zilizo na sera za kujipima VVU iliongezeka kutoka mataifa sita hadi 88 - na mataifa mengine 31 yanaandaa será hizo. 

Kujipima VVU kumesaidia kufikiwa idadi kubwa ya watu wakiwemo wanaume na vijana ambao wana uwezekano mdogo wa kufikia vituo vya afya na walikuwa na viwango vya chini vya upimaji na walengwa wakuu wanaolengwa kutumia vifaa hivyo ni wale ambao husita kutembelea vituo vya afya kwa sababu ya unyanyapaa au ubaguzi.

 Mkurugenzi Mkuu wa UNITAID Dkt Philippe Duneton, anafafanua kuhusu nukta hiyo kwa kusema, “Vifaa ni muhimu sana, lakini vifaa ambavyo watu wanaweza kutumia peke yao ni muhimu zaidi hasa katika hali ya hivi sasa ya COVID-19, kwa sababu imekuwa vigumu zaidi kwenda katika hospitali na vituo vya afya."