Dec 02, 2021 07:08 UTC
  • Wamarekani wengi wana wasiwasi wa kutokea vita kati ya nchi yao na China

Uchunguzi wa maoni uliofanyika nchini Marekani unaonyesha kuwa raia wengi wana hofu ya kutokea vita baina ya nchi hiyo na China katika miaka mitano ijayo.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Reagan karibu asilimia 71 ya Wamarekani wana wasiwasi wa kutokea vita kati ya Marekani na China katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanaonyesha kuwa, ni asilimia 14 tu ya waliotoa maoni yao wanaihisi Russia ndio tishio kwa nchi yao huku asilimia 12 wakiitaja Korea Kaskazini.

Vilevile asilimia 71 ya waliotoa maoni yao wamesema, ikiwa Taiwan itashambuliwa na China, Marekani itapasa ikitambue kisiwa hicho kuwa ni nchi huru.  Asilimia 55 ya washiriki wa uchunguzi huo wamesema, suhula za kijeshi za Marekani zikiwemo manowari za kubebea ndege inapasa zipelekwe katika eneo la langobahari la Taiwan huku asilimia 50 wakitaka Marekani iitangaze anga ya Taiwan eneo lililopigwa marufuku ndege kupaa hata kama kufanya hivyo kutamaanisha kuzitungua ndege za kivita za China.

Pamoja na hayo, asilimia 66 ya Wamarekani wameunga mkono kuiwekea China vikwazo vya kiuchumi huku asilimia 40 wakitaka vikosi vya nchi kavu vya jeshi la Marekani vitumiwe kuilinda Taiwan.

Ijapokuwa asilimia ya 71 walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Reagan wana wasiwasi wa kutokea vita baina ya Marekani na China katika miaka mitano ijayo, huku asilimia 61 wakihofia kutokea vita vya nyuklia, lakini Wamarekani wengi zaidi wana wasiwasi wa kutokea maafa mengine. Asilimia 88 wana hofu ya kufanyika hujuma za intaneti, asilimia 82 wanachelea kutokea mashambulio ya kigaidi na asilimia 81 wana wasiwasi wa kuzuka janga jengine la ugonjwa wa dunia nzima katika kipindi hicho cha miaka mitano ijayo.../

Tags