Dec 02, 2021 08:26 UTC
  • Siku ya tatu ya mazungumzo ya Vienna

Mazungumzo yanayolenga kuiondolea Iran vikwazo vya kiuchumi, yaliendelea Jumatano huko Vienna Austria kwa siku ya tatu mfululizo kati ya Iran na nchi za kundi la 4+1 ambazo ni Ujerumani, Ufaransa, Uinngereza, Russia na China.

Katika mazungumzo hayo ujumbe wa Iran umekutana na kufanya mazungumzo na pande zote husika kwa ajili ya kudhaminiwa haki za taifa la Iran na kutofumbiwa macho waliohusika na mkwamo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Iran inasisitiza kuwa maudhui mbili za vikwazo na uwajibikaji wa nyuklia katika mapatano hayo hazipasi kufanywa mateka wa upande wa pili na kwamba kuna udharura wa kwanza kuondolewa vikwazo ambavyo vilisababishwa na hatua ya Marekani kujiondoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo. Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anasema kuhusu suala hilo kwamba: Mazungumzo ya Vienna ambayo kipaumbele chake cha msingi ni kuondolewa vikwazo yanaendelea kwa nguvu zote. Iwapo nchi za Magharibi zitaonyesha nia njema, mapatano mazuri yanaweza kufikiwa.

Hussein Amir Abdollahian

Licha ya mazungumzo ya vienna kufanyika katika mazingira mazuri ya maelewano ya awali, lakini inaonekana kuna baadhi ya pande ambazo zinashinikizwa na Marekani ili kuyalekeza mazungumzo upande mbaya na hatimaye kutofikiwa natija ya mwisho. Ni kwa msingi huo ndio maana baadhi ya pande zinazotiliwa shaka zikataka yahitimishwe haraka hata bila ya kufikiwa malengo yanayokusudiwa. Hii ni katika hali ambayo ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ambao umeingia kwenye mazungumzo hayo kwa malengo maalumu na yaliyoainishwa kabla unayafuatilia kwa umakini na nguvu zake zote na wala hautaruhusu haki za taifa la Iran zikanyagwe kwa kisingizio cha kufuata wakati au ratiba iliyopangwa.

Jambo jingine ambalo linaweza kuacha taathira hasi katika mazungumzo ya Vienna ni hitilafu za kisiasa zinazoendelea nchini Marekani. Katika siku za karibuni wabunge 25 wa chama cha Republican walimwandikia barua Rais Joe Biden wa Marekani wakisema watapinga hatua yoyote ya Iran kuondolewa vikwazo na kuwa iwapo watapata wingi wa kura kwenye Congress watapitisha sheria ya kutekeleza mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya taifa la Iran.

Kutokuwepo sauti moja katika siasa za nje za Marekani na vilevile historia ndefu ya nchi hiyo katika kukiuka sheria za kimataifa, mfano mzuri wa hilo ikiwa ni hatua ya nchi hiyo ya kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano ya JCPOA mwaka 2018, ni suala ambalo limeongeza wasi wasi wa mazungumzo ya Vienna kutofikia natija inayokusudiwa. Ni kwa msingi huo ndipo Iran ikawa inasisitiza kwamba kabla Marekani kuruhusiwa kurejea katika mapatano ya JCPOA inapasa kulazimishwa kutoa dhamana kuwa haitakiuka tena mapatano hayo na kwamba iwapo hilo litatokea basi upande wa pili nao utakuwa na ruhusa ya kisheria ya kulipiza kisasi na kuchukua hatua zinazoambatana na kitendo kama hicho cha Marekani.

Donald Trump akitangaza kuindoa Marekani katika mapatano ya JCPOA

Katika uwanja huo, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran anasema: Serikali ya Iran inashiriki katika mazungumzo ya Viena kwa nia njema na kwa nguvu zake zote ili kuhakikisha kwamba mapatano yatakayofikiwa katika mazungumzo hayo yatapelekea kuondolewa vikwazo. Ni wazi kuwa iwapo upande wa pili nao utashiriki kwenye mazungumzo kwa njia njema ya kuwezesha Iran iondolewe vikwazo, na si kwa lengo la kupoteza wakati tu na kutoa visingizio visivyo na msingi, tunaweza kusema kuwa mazungumzo yako kwenye mkondo mzuri unaokubalika.