Dec 03, 2021 07:52 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Watu milioni 274 kuhitaji msaada wa dharura mwaka ujao

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watu wapatao milioni 274 duniani kote watahitaji msaada wa dharura na ulinzi mwaka ujao wa 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka huu.

Umoja wa Mataifa umetangaza hilo baada ya kufanya tathmini ya hali ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Tathimini hiyo inakadiria kwamba, dola bilioni 41 zinahitajika kutoa misaada na ulinzi kwa watu milioni 183 wanaohitaji zaidi msaada huo.

Sehemu moja ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, mizozo ya muda mrefu inaendelea, na ukosefu wa utulivu na usalama umekuwa mbaya zaidi katika sehemu kadhaa za dunia, hususan Ethiopia, Myanmar, na Afghanistan, na pia bila shaka janga la COVID-19 ambalo tumekumbushwa hivi karibuni kwamba halijaisha huku nchi maskini zikikosa chanjo.

Kulingana na ripoti hiyo ya mtazamo wa hali ya kibinadamu duniani, zaidi ya asilimia moja ya watu duniani wamekimbia makazi yao na umaskini uliokithiri unaongezeka tena.

 

Inaelezwa kuwa, katika majanga mengi, wanawake na mabanati wanateseka zaidi, kwani kuna ongezeko kubwa la kukosekana kwa usawa wa kijinsia na hatari za kutokuwa na ulinzi.

Mwezi uliopita Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilitangaza kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa katika nchi 43 duniani imeongezeka hadi kufikia milioni 45, wakati njaa ikiongezeka kote ulimwenguni.

Mwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ongezeko hilo linatokana na wale ambao wanaishi katika maeneo yaliyowekwa katika kiwango cha njaa 4 yaani IPC4 na zaidi, kama vile nchini Afghanistan, pamoja na ongezeko nchini Ethiopia, Haiti, Somalia, Angola, Kenya na Burundi.