Dec 03, 2021 12:59 UTC
  • Israel na Marekani vizuizi vikuu vya kuwepo Mashariki ya Kati isiyo na silaha za maangamizi ya umati

Fikra ya kuwepo Mashariki ya Kati isiyo na silaha za mauaji ya halaiki ilitolewa miaka kadhaa iliyopita lakini hadi sasa fikra hiyo haijatekelezwa kivitendo.

Mkutano wa pili wa Mashariki ya Kati Isiyo na Silaha za Mauaji ya Umati ulianza Jumatatu wiki hii kwa hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika sekretarieti ya umoja huo mjini New York huko Marekani. Mashariki ya Kati isiyo na silaha za maangamizi ni fikra iliyosalia kwenye makaratasi tu bila ya kutekelezwa na kuna sababu mbili za jambo hilo ambazo zote zinahusiana na Marekani na utawala haramu wa Israel.

Sababu ya kwanza ni mienendo na tabia ya Marekani. Marekani ni muungaji mkono mkuu wa wazo la Mashariki ya Kati isiyo na silaha za maangamizi, lakini kivitendo Washington haijachukua hatua yoyote katika uwanja huo, na kinyume chake, imechukua hatua ya kuimarisha sera za kijeshi katika eneo la Asia Magharibi. Marekani pia ndiyo muuzaji mkubwa zaidi wa silaha katika eneo la Magharibi mwa Asia na ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ndio pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika eneo hilo. Utawala wa Washington pia una mtazamo wa kibaguzi kuhusu suala la nyuklia duniani, hasa katika eneo la Magharibi mwa Asia. Kwa mfano tu, wakati serikali ya Marekani inapinga harakati za Iran za kupata nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani na inatumia suala hilo kama kisingizio cha kuiwekea Iran mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi, nchi hiyo hiyo imekaa kimya kuhusu harakati za Saudi Arabia za kupata nishati ya nyuklia, na baadhi ya vyanzo vinasema kuwa Saudia inafanya shughuli za siri za nyuklia.

Mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman

Wakati huo huo, Marekani haikuhudhuria mkutano wa sasa wa Mashariki ya Kati Isiyo na Silaha za Maangamizi mjini New York, jambao ambalo liekosolewa pia na Russia. Kuhusiana na hilo, Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika mashirika ya kimataifa yenye makao huko Vienna, ametuma ujumbe kwenye Twitter uliokuwa na picha ya meza tupu ya Marekani katika mkutano huo, akikosoa kutokuwepo kwa Washington kwenye mkutano Mashariki ya Kati Bila ya Silaha za Maangamizi. Ulyanov ameandika: "Kiti kitupu katika mkutano wa kuanzishwa eneo lisilo na Silaha za maangamizi ya halaiki katika Mashariki ya Kati. Inasikitisha kwamba Marekani kama moja ya nchi tatu zilizounga mkono azimio la 1995 ambalo lina jukumu maalumu katika utekelezaji wa wazo hilo, imekataa mwaliko wa kuhudhuria mkutano huu."

Sababu ya pili ni mienendo ya utawala haramu wa Israel. Utawala huo ambao kama tulivyotangulia kusema ndio pekee unaomiliki silaha za nyuklia Asia Magharibi, umeendelea kukataa kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na unakwepa kushiriki katika vikao na mikutano inayojadili Mashariki ya Kati isiyo na silaha za maangamizi ya umati. Kuhusiana na suala hilo, Majid Takht-Ravanchi, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisema katika mkutano wa pili wa Mashariki ya Kati Isiyo na Silaha za Maangamizi Umati kwamba: "Mafanikio ya mkutano huu hayazifurahishi baadhi ya tawala. Nchi zote zilizoalikwa zikiwemo nguvu kuu nne za nyuklia zinashiriki katika mkutano huu lakini Marekani na utawala haramu wa Israel zinaendelea kuupinga na hazikushiriki. Katika hali na mazingira kama haya, njia ya kwanza ya kuondoa vizuizi hivi ni Israel kujiunga na NPT na kukubali ukaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika shughuli zake zote za nyuklia. Kwa hakika suala la kuanzishwa Mashariki ya Kati isiyo na silaha za nyuklia limeshindikana kutokana na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Israel.”

Majid Takht-Ravanchi

Nukta ya mwisho ni kwamba, mikutano inaojadili maudhui ya Mashariki ya Kati isiyo na silaha za maangamizi itakuwa na matunda pale madola makubwa, hasa Marekani, yatakapokuwa na nia ya dhati ya kutimiza kivitendo fikra hiyo na kuvunja kimya chao kuhusiana na silaha za nyuklia za Israel.  

Tags