Dec 04, 2021 02:37 UTC
  • Russia yasisitiza kuizuia Nato ili isipanue uwepo wake mashariki mwa Ulaya

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesisitiza kwamba kuna haja ya kuzuia Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) kupanua uwepo wake mashariki mwa bara Ulaya.

Maria Zakharova jana Ijumaa alisema kuwa Moscow inataka kufikia mapatano na muungano wa Nato ambayo yatauzuia muungano huo kupanua uwepo wake mashariki mwa Ulaya hususan karibu na mipaka ya Russia.

Zakharova ameashiria kwamba tangu baada ya kumalizika vita baridi Russia imekuwa ikipewa ahadi za mara kwa mara za Nato kwamba muungano huo hautajiimarisha zaidi mashariki mwa Ulaya wala kukaribia mipaka ya nchi hiyo na kueleza kuwa, ahadi zote hizo zimesahaulika na hazijatekelezwa hadi sasa.  

Viongozi wa Ukraine na wa nchi za Magharibi hivi karibuni waliibua chokochoko dhidi ya Russia wakidadi kuwa Moscow imetuma wanajeshi wake katika mpaka na Ukraine na kwamba kuna uwezekano Russia ikaishambulia Ukraine. 

Russia kwa upande wake imeelezwa wazi mara kadhaa kuwa harakati zake za kijeshi katika mpaka baina yake na Ukraine ni za kawaida.  Hata hivyo Marekani na waitifaki wake wanajaribu kuidhihirisha hali ya mambo katika mpaka wa Russia na Ukraine kuwa iliyojaa mvutano na wasiwasi.  

Njama za Marekani za kuigombanisha Ukraine na Russia 

 

Tags