Dec 04, 2021 07:38 UTC
  • Blinken akiri Marekani ilitengwa baada ya kujiondoa JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amekiri kuwa, nchi yake ilitengwa baada ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).

Katika mahojiano na Shirika la Habari la Reuters  Anthony Blinken ameongeza kuwa: "Kujiondoa Washington katika JCPOA lilikuwa kosa kubwa wakati wa urais wa Donald Trump."

Katika mahojiano hayo, Blinken amekariri matakwa yaliyokuzwa kupita kiasi ya Marekani kwa Iran na mapatano ya JCPOA huku akidai kuwa Iran haina azma imara katika mazungumzo ya Vienna.

Trump alijiondoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 2018 akidai kuwa mapatano hayo ya kimataifa ya mwaka 2015 ambayo yaliidhinishwa na rais aliyemtangulia, Barack Obama, yalikuwa 'mabaya zaidi' katika historia.

Wiki hii mji mkuu wa Austria, Vienna umekuwa mwenyeji wa mazungumzo baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewea vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya Iran. Nchi za 4+1 ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.

Ali Bagheri-Kani Mkuu wa Timu ya Iran katika Mazungumzo ya Kuondoa Vikwazo vya Kidhalimu dhidi ya Iran na ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewaslisha matini ya pendekezo lake kwa kundi la 4+1.

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa kundi la 4+1, Umoja wa Ulaya na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu wiki hii walisisitiza kuwa upande wa Iran umekubaliana kwamba suala la kuondoa vikwazo vya kidhalimu na haramu vya Marekani dhidi ya Iran lifuatiliwe kwa uzito maalumu.