Dec 04, 2021 14:36 UTC
  • Kuongezeka kwa mzozo kati ya Russia na Magharibi juu ya Ukraine na upanuzi wa NATO kuelekea Mashariki

Katika wiki za hivi karibuni, makabiliano kati ya Russia na Magharibi kuhusu Ukraine yamechukua sura mpya, huku pande mbili zikitoa maonyo ya mara kwa mara kuhusu hatua zozote za kijeshi.

Katika hatua ya hivi karibuni, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksiy Raznikov alidai Ijumaa ya jana kwamba Russia imetuma zaidi ya wanajeshi 94,000 karibu na mpaka wa nchi hiyo, na kwamba yumkini inajitayarisha kwa ajili ya mashambulizi makubwa dhidi ya Ukraine kufikia mwisho wa Januari 2022. Wizara ya Ulinzi ya Ukraine pia ilidai Jumanne wiki hii kwamba, wanajeshi wa Russia walikuwa katika hali ya tahadhari kwenye mpaka wa mashariki mwa nchi hiyo na kwamba wanafanya mazoezi makubwa katika eneo hilo. Wakati huo huo Russia imesema jeshi la Ukraine linajiandaa kwa operesheni kubwa ya kijeshi katika eneo linaloshikiliwa na wapinzani mashariki mwa nchi hiyo. Moscow imeitahadharisha Kiev kuhusiana na suala hilo.

Kwa sasa kambi ya nchi za Magharibi, katika kalibu ya jumuiya ya NATO, inatumia mzozo wa Ukraine na Russia kuzidisha shinikizo kwa Moscow, hususan katika siku za hivi karibuni, kufuatia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO, ambapo Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo ya kijeshi na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani wametoa matamshi makali ya kukabiliana na hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Ukraine. Russia imesema mara kwa mara kwamba hatua zake za kijeshi kwenye mpaka na Ukraine ni za kawaida, na kwamba Marekani na washirika wake wanataka kuzidisha mvutano kwenye mpaka wa Russia na Ukraine.

Swali linalojitokeza ni kwamba, je, kwa kutilia maanani kwamba Ukraine si mwanachama wa NATO, jumiya hiyo inatumia msingi gani kutoa onyo la kujibu hatua zozote za kijeshi zinazoweza kufanywa na Russia dhidi ya Ukraine? Kimsingi, ni kwa nini Marekani na NATO zimekuwa na kiwango kikubwa cha majeshi karibu na Russia na maeneo yake ya mpakani katika miaka ya hivi karibuni?

Washington na NATO zimekuwa zikizunguzia mara kwa mara madai ya tishio la Russia dhidi ya Ulaya, ingawa ukweli ni kwamba, kupitia ya fremu ya sera yake ya kujipanua zaidi upande wa Mashariki katika miongo miwili iliyopita, NATO imekuwa ikifanya juhudi za kuzipa uanachama nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki na kisha Balkan ya Magharibi katika jumuiya hiyo ya kijeshi na hususan nchi majirani wa Russia kama Ukraine na Georgia. Lengo kuu la NATO ikioongozwa na Marekani, ni kuidhibiti kikamili Russia bali kuizingira nchi hiyo. Suala hili limepingwa vikali na Moscow, ambayo inaliona kama mstari mwekundu kwa usalama wa taifa wa Russia. Mchambuzi wa masuala ya siasa, Saeed Davar anasema: "Uwepo na kujipanua NATO huko Ulaya Mashariki kuelekea Russia ni tishio kwa usalama wa taifa la Warusi, na kutokabiliana na hatua hizi za kujipanua kunashusha hadhi ya Russia katika mahusiano ya kimataifa na kuiruhusu NATO kuwa karibu zaidi na mipaka ya nchi hiyo." Katika msimamo wa hivi karibuni kabisa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov alisema Alkhamisi iliyopita kwamba: "Mipango ya NATO ya kutaka kuzijumuisha nchi za Georgia na Ukraine katika jumuiya hiyo ya kijeshi ni bomu la masaa katika moyo wa bara Ulaya." 

Sergey Lavrov

Onyo hili kali lililotolewa na afisa wa ngazi za juu kabisa wa siasa za kigeni wa Russia linaonyesha wasiwasi wa Moscow kuhusu juhudi za NATO kuiunganisha Ukraine katika shirika hilo la kijeshi. Russia imetangaza mara kwa mara kwamba, inataka kufikia mapatano na muungano wa NATO ambayo yatauzuia muungano huo kupanua uwepo wake mashariki mwa Ulaya hususan karibu na mipaka ya Russia. Rais wa Russia Vladimir Putin amesisitiza kuwa upanuzi wa NATO upande wa mashariki haukubaliki na kwamba dhamana ya kisheria inahitajika kwamba suala hilo halitafanyika. Russia imekuwa ikipewa ahadi za mara kwa mara za NATO kwamba muungano huo hautajiimarisha zaidi mashariki mwa Ulaya wala kukaribia mipaka ya nchi hiyo; hata hivyo ahadi hizo, kama zilivyo ahadi nyingine za nchi za Magharibi, zimesahaulika na hazijatekelezwa hadi sasa.  

Tags