Dec 08, 2021 02:33 UTC
  • Kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela Aung San Suu Kyi

Mahakama nchini Myanmar imemhukumu kifungo cha miaka minne jela Aung San Suu Kyi kiongozi wa kilichokuwa chama tawala nchini humo cha National League for Democracy (NLD).

Kiongozi huyo wa Myanmar aliyeng'olewa madarakani mapema mwaka huu amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela, ikiwa ni hukumu ya kwanza ya msururu wa kesi zinazomkabili ambazo zinazoweza kumfunga maisha jela. Kwa mujibu wa mahakama hiyo, Aung San Su Kyi amepatikana na hatia ya uchochezi na kuvunja maagizo na miiko ya kukabiliana na msambao wa maradhi ya COVID-19.

Mshitakiwa mwenza katika kesi hiyo Win Myint, Rais wa zamani ambaye pia ni mshirika katika chama cha Aung Suu Kyi cha National League for Democracy (NLD)  naye amehukumiwa kwenda jela miaka minne gerezani kwa makosa sawa na ya Aung Suu Kyi katika kesi ya aina yake.

Hii ni katika hali katika hali ambayo, sambamba na hukumu hiyo Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa: Hatua ya majenerali wa jeshi wanaotawala nchini Myanmar ya kumhukumu kifungo jela Aung San Suu Kyi kiongozi aliyekuwa na ushawishi mkubwa, wameibadilisha nchi hiyo na kuifanya kuwa gereza na wanachokiafuatilia ni kuwakandamiza watu wanaopigania uhuru wa kutoa maoni.

Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo. Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020) ambapo chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi. 

Aung San Suu Kyi

 

Hukumu ya miaka minne jela dhidi ya Aung San Suu Kyi imetolewa katika hali ambayo, jamii ya kimataifa ilitaraji watawala wa kijeshi nchini Myanmar kama walivyoahidi wangetekeleza ahadi zao za kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi wa Bunge huru na wa haki.

Kikawaida hatua muhimu inayopaswa kuchukuliwa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi katika nchi yoyote ambapo lengo ni kuheshimu haki ya wananchi ya kujiamulia hatima na mustakabali wao ni kuandaliwa mazingira ya vyama na makundi yote ya kisiasa kushiriki katika uchaguzi.

 Licha ya ukosoaji unaomuandama Aung San Suu Kyi katika kipindi cha utawala wa chama chake cha National League for Democracy (NLD) hususan ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa dhidi ya jamii ya wachache ya Waislamu wa Kirohingya, lakini tuhuma za kufanya uchochezi na kukiuka miiko na sheria za kukabiliana na Corona si hatua ya kuhalalishika; na kumfunga jela miaka 4 San Suu Kyi kwa tuhuma kama hizi ni jambo ambalo halikubaliki si ndani ya Myanmar wala mbele jamii ya kimataifa na asasi za haki za binadamu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, tuhuma za kimsingi anazokabiliwa nazo Aung San Suu Kyi na viongozi wa kilichokuwa tawala nchini Myanmar na ambazo zilitumiwa na jeshi kama kisingizio kwa ajili ya kufanya mapinduzi ni udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi wa Bunge. Lakini Aung San Suu Kyi na mshirika wake wamefungwa jela kwa tuhuma za machafuko, kuchochea fujo na kukiuka sheria za Corona.

Maandamano ya wananchi wa Myanmar ya kupinga utawala wa kijeshi

 

Hukumu dhidi ya San Suu Kyi inaonyesha kuwa, licha ya nara za wanajeshi wanaotawala Myanmar za kufungua anga ya siasa ya nchi hiyo, lakini nchi hiyo ingali katika njia ya kufungwa anga ya kisiasa, hatua ambayo inashadidishha wasiwasi wa kutekelezwa ahadi za majenerali hao za kukabidhi madaraka ya nchi kupitia mchakato wa uchaguzi huru wa Bunge.

Kuna mtazamo huu kwamba, jeshi la Myanmar ambalo lipo chini ya mashinikizo makubwa ya kisiasa ya ndani na ya nje, huenda mwisho wa siku likaitisha uchaguzi kwa ajili ya kupunguza mashinikizo na hivyo kuvibana na kuviweka kando vyama vikuu vya siasa kwa kisingizio cha kuhatarisha usalama wa taifa na wakati huo huo kuvifungulia uwanja vyama na makundi ya kisiasa ambayo yana mfungamano na wanajeshi hao  na hivyo kuhakishha washirika wao hao wanaingia madarakani.

Tags