Dec 08, 2021 02:34 UTC
  • WHO: Corona imechangia kuongezeka vifo vya malaria duniani

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuvurugika utoaji wa huduma za afya kutokana na janga la Corona kulipelekea kuongezeka vifo vya wagonjwa wa malaria duniani mwaka jana 2020.

WHO imesema hayo katika ripoti yake ya kila mwaka kuhusu malaria na kufafanua kuwa, watu 69, 000 zaidi waliaga dunia mwaka uliopita kutokana na taathira hasi za ugonjwa wa COVID-19 kwa mifumo ya afya katika pembe mbali mbali za dunia.

Katika ripoti hiyo, WHO imesema kwa ujumla watu 627, 000, aghalabu yao wakiwa watoto wadogo wa nchi maskini za Afrika, waliaga dunia mwaka jana kutokana na malaria, ikilinganishwa na watu 558, 000 mwaka juzi 2019.

Ripoti hiyo ya malaria ulimwenguni inaonyesha maendeleo dhidi ya malaria yanaendelea kupungua, hasa katika nchi zenye mzigo mkubwa barani Afrika.

Mbu anayeeneza ugonjwa wa malaria

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, ugonjwa wa malaria unaua zaidi ya ugonjwa wa COVID-19 katika nchi za Afrika.

Shirika la Afya Duniani limesema idadi ya watu walioaga dunia kwa malaria ni kubwa zaidi, ikilinganishwa na watu 224 000 walioaga dunia kwa Corona barani Afrika kufikia sasa.

Tags