Dec 08, 2021 02:56 UTC
  • Mtuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi atiwa mbaroni mjini Paris Ufaransa

Vyombo mbalimbali vya habari vimetangaza kuwa, mtuhumiwa mmoja wa mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliyekuwa akiikosoa serikali ya Saudia, ametiwa mbaroni mjini Paris Ufaransa wakati alipokuwa njiani kuelekea Riyadh, Saudi Arabia.

Redio ya RTL ya Ufaransa imetangaza kuwa, mtuhumiwa huo ni afisa wa zamani wa kikosi cha ulinzi cha ufalme wa Saudi Arabia na amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris wakati alipokuwa safarini kuelekea Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia.

Kwa upoande wake Euro News imesema kwamba imewasiliana na polisi ya taifa ya Ufaransa na kuthibitisha kuwa, Khalid Alotaibi, 33, ametiwa mbaroni na polisi wa mpakani alipokuwa anajiandaa kupanda ndege kuelekea Riyadh. 

Polisi ya Ufaransa imesema, imemtia mbaroni Alotaibi kutokana na waranti uliotolewa na Uturuki kupitia polisi ya kimataifa ya Interpol.

Mafiki wa Khashoggi kote ulimwenguni

 

Jamal Khashoggi aliuliwa kikatili na kinyama mwaka 2018 ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul Uturuki na kikosi maalumu cha wauaji makatili kilichotumwa maalumu kutoka Saudi Arabia. Mwili wake uliokatwa vipande vipande na timu hiyo maalumu ya mauaji ya Saudia, haujapatikana hadi leo hii.

Nchi za Magharibi zinasema, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman ndiye aliyetoa amri ya kufanyika mauaji hayo. Mauaji hayo yaliushitua vibaya ulimwengu na kuharibu mno sura ya Saudi Arabia hususan mrithi wa kiti cha ufalme bin Salman na hasa nje ya nchi hiyo.

Afisa huyo wa gadi ya kifalme ya Saudi Arabia ametiwa mbaroni nchini Ufaransa siku chache tu tangu rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron alipoonana na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia Mohammed bin Salman mjini Jeddah.