Dec 08, 2021 02:56 UTC
  • Mkuu wa CIA akiri kuwa mpango wa nyuklia wa Iran hauna malengo ya kijeshi

Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA amekiri kuwa mpango wa nyuklia wa Iran hauna malengo ya kijeshi.

William Burns amesema, hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa viongozi waandamizi wa Iran wameamua kuuelekeza mpango wa nyuklia wa nchi hiyo kwenye malengo ya kijeshi.

Kabla ya kauli hiyo ya Burns, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikwisha tangaza na kusisitiza mara kadhaa kuwa, mpango wake wa nyuklia ni wa malengo ya amani.

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) nao pia umesisitiza katika ripoti zake unazotoa mara kwa mara kwamba Iran inaendelea kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha shughuli zake za nyuklia hazikengeuki malengo ya amani.

Lakini licha ya mkuu huyo wa CIA kutoa kauli hiyo, na bila kuashiria chochote kuhusu hatua ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya yuklia ya JCPOA na kwamba vikwazo vya nchi hiyo dhidi ya Iran ndicho kikwazo kikuu cha mazungumzo ya nyuklia ya mjini Vienna, amedai kuwa, kwa sasa Tehran haijaonyesha kwamba inayapa uzito mazungumzo hayo.

Duru mpya ya mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa ilianza siku ya Jumatatu iliyopita ya tarehe 29 Novemba mjini Vienna.

Katika mazungumzo yanayoendelea hivi sasa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewapatia wadau wa upande wa pili wa mazungumzo hayo hati mbili zinazohusu kuondolewa vikwazo vya Marekani na nchi hiyo kuhakikisha inatekeleza majukumu yake katika JCPOA.

Nchi zinazofanya mazungumzo na Iran, ambazo zinaunda kundi la 4+1, yaani Ufaransa, Uingereza, Russia, China na Ujerumani zimetangaza kuwa, ili ziweze kutoa majibu yenye hoja, ushahidi na ya kimantiki kwa mapendekezo yaliyotolewa na Jamhuri ya Kiislamu, zinahitaji kwenda kushauriana na serikali zao.

Kwa muktadha huo zimepatiwa fursa ya kwenda kufanya mashauriano hayo ili baadaye zirudi mjini Vienna kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo.../

Tags