Dec 08, 2021 14:26 UTC
  • New York Post: Biden ni dhaifu, hawezi kukabiliana na Russia, China na Iran

Gazeti la Marekani la New York Post limemtaja rais wa sasa wa nchi hiyo kuwa ni dhaifu na mwenye kutetereka na kwamba hawezi kukabiliana na Russia, China na Iran katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Katika makala yake ya leo Jumatano, New York Post limechambua miezi 11 ya utawala wa Joe Biden nchini Marekani na kuandika kuwa, katika kipindi hicho kiongozi huyo ameonekana dhaifu na asiyefaa.

Gazeti hilo limeashiria mivutano ya kimataifa iliyopo hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya dunia ukiwemo ule wa Ukraine na Russia na kusema: Joe Biden ni mmoja kati ya marais dhaifu zaidi katika historia ya Marekani na hana uwezo wa kukabiliana na Russia, China na Iran. 

Likitoa vielelezo vya udhaifu wake, gazeti la New York Post limeandika kuwa, Biden ameshindwa hata kuunganisha chama chake katika Kongresi ya Marekani, na wajumbe wa chama hicho hawaoni ulazima wowote wa kupasisha miswada inayopendekezwa na kiongozi huyo.

New York Post limeitaja maudhui ya Afghanistan kuwa ndiyo kielelezo cha utendaji dhaifu zaidi wa Joe Biden katika miezi kadhaa iliyopita tangu aliposhika madaraka ya nchi na kuandika kuwa: Kuondoka kiholela na bila ya mpangilio maalumu kwa jeshi la Marekani nchini Afghanistan kumeonesha kuwa, Biden anataka kuwaacha mkono marafiki na waitifaki wa Marekani.

Kuhusu mazungumzo ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, gazeti hilo limeandika kuwa, Iran imekuwa jasiri sana kiasi kwamba imekataa kukutana na kuzungumza na mwakilishi wa Marekani katika mazungumzo hayo na imemlazimisha Biden alegeze kamba. 

Tags