Dec 09, 2021 04:41 UTC
  • Iran yalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya mahakama ya ICC

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Sayyid Mehdi Hosseini Esfidvajani, Mwakilishi wa Iran katika Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Roma Uliobuni mahakama hiyo (ASP) amesema hayo katika hotuba yake kwa mkutano wa 20 wa taasisi hiyo mjini Hague nchini Uholanzi. Mkutano huo ulianza Disemba 6 na unatazamiwa kumalizika Disemba 11.

Afisa huyo wa Iran ameeleza bayana kuwa, kitendo cha Marekani cha kuwawekea vikwazo maafisa wa mahakama hiyo ya kimataifa kinakiuka wazi wazi sheria za kimataifa.

Sayyid Esfidvajani amebainisha kuwa, mienendo hii ya Marekani ya kutumia vikwazo kama silaha inalenga kudunisha uhuru wa taasisi za kimataifa.

Amefafanua kwa kusema, Marekani ilitumia mbinu zake hizo za kibeberu dhidi ya ICC na maafisa wake ili kutoa fursa kwa wanajeshi wake kuondoka Afghanistan, na hivyo kuandaa mazingira ya kutokamatwa na kufikishwa mbele ya sheria watekelezaji wa jinai za kivita miongoni mwa askari hao.

Mwakilishi wa Iran katika Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Roma Uliobuni ICC ameongeza kuwa, mahakama hiyo ya mjini Hague inapaswa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na taathira hasi na haribifu za ukiukwaji wa sheria za kimataifa kutokana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani.

 

Tags