Dec 09, 2021 04:44 UTC
  • Marekani yasusia kidiplomasia michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi nchini China

Jen Psaki Msemaji wa Ikulu ya White House alitangaza Jumatatu usiku kuwa, "serikali ya Joe Biden haitatuma mwakilishi rasmi au wa kidiplomasia katika michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi." Amedai kuwa sababu ya uamuzi huo wa serikali ya Marekani ni mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu katika mkoa wa Xinjiang na vitendo vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu China.

Psaki ameendelea kusema kuwa: "Kama ambavyo Biden alimfahamisha Rais Xi Jinping wa China katika mazungumzo, utetezi wa haki za binadmau uko ndani ya DNA ya Marekani." 

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin amekosoa vikali hatua ya Marekani kuingiza siasa katika michezo na kusema hatua hiyo ya utawala wa Marekani ni kinyume cha Hati ya Michezo ya Olimpiki. Amesema China haitawaalika wanasiasa wa nchi  za Magharibi ambao wamezungumza kuhusu kususia michezo hiyo ya Olimpiki ya msimu wa baridi.

Hatua mpya ya Marekani ya kususia kidiplomasia michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi nchini China ni uhasama wa hivi karibuni zaidi wa Washington dhidi ya Beijing. Kisingizo cha ususiaji huo kimetangazwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu katika mkoa wa  Xinjiang. Msemaji wa Ikulu ya White House amedai kuwa utetezi wa haki za binadmau uko katika dhati au DNA ya Marekani katika hali ambayo nchini Marekani kwenyewe wananchi wanakumbwa na hali mbaya sana ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Jen Psaki Msemaji wa Ikulu ya White House

Utawala wa Biden umekuwa ukidai kuwa unaunga mkono haki za binadmau lakini sasa utawala huo unatumia haki za binadamu kama chombo cha kukosoa na kuziwekea vikwazo nchi mahasimu wake kama vile China na Russia. Kufuatia madai ya msemaji wa Ikulu ya White House, inasuburiwa kuona iwapo utawala wa Biden utachukua hatua za kukabiliana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Marekani kwenyewe au la.

Taasisi za kutetea haki za binadamu hasa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa mara kadhaa zimechapisha ripoti kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Marekani. Mifano ya ukiukwaji wa haki za binadamu Marekani ni ubaguzi wa rangi hasa dhidi ya watu wenye asili ya Afrika, ukiukwaji wa haki za wafungwa ambao wengi ni wale wenye asili ya Afrika,  ukiukwaji wa haki za Wamarekani asili, ukiukwaji wa haki za wanawake na kutendewa maovu wahajiri wa kigeni. Aidha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeashiria ubaguzi wa rangi ambao ni rasmi nchini Marekani na kutaka hali hiyo ibadilishwe katika nchi hiyo. Pamoja na hayo lakini Marekani inadai kuwa eti ni kinara wa kutetea haki za binadamu duniani na imekuwa ikipuuza matakwa ya taasisi za kimataifa za kutetea haki za binadamu.

Kwa hivyo wakati ambao Marekani haina ustahiki wa kutoa hukumu kuhusu hali ya haki za binadamu katika nchi zingine, kila mwaka husambaza ripoti kuhusu hali ya  haki za binadamu katika nchi ambali mbali hasa zile ambazo ni mahasimu wake kama vile China.

Inaelekea kuwa, wigo wa makabiliano na malumbano baina ya Marekani na China umeingia katika awamu mpya wakati wa utawala wa Biden na kususiwa kidiplomasia michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi ni dalili ya kuharibika zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.

Wakuuu wa serikali ya Biden wameitaja China kuwa changamoto kubwa zaidi ya Marekani katika uga wa kijiostratijia katika karne ya 21. Mtazamo huo unaashiria mtazamo jumla wa Washington kuhusu ushawishi wa China katika eneo la Indo-Pasikifi na dunia nzima kwa ujumla.

Rais wa China, Xi Jinping (kushoto), na Rais wa Marekani Joe Biden,

Hofu kuu ya Washington haiko katika tuhuma zake za kukaririwa dhidi ya China bali kile ambacho hasa kinaiingiza Marekani kiwewe ni kuwa katika mustakabali wa karibu, China itakuwa dola linaloongoza kiuchumi duniani na sambamba na hilo pia nguvu za kijeshi za nchi hiyo zinazidi kuongezeka. Nukta hizo mbili zitabadilisha mahesabu ya mlingano wa kijeshi na kuibua changamoto kwa Marekani katika eneo la Asia Mashariki. Kwa msingi huo Marekani inatumia kila fursa kuidhoofisha China.

Fyodro Lukyanov, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Makabilianao makali ya kiuchumi baina ya Marekani na China yanaweza kugeuka na kuwa makabiliano ya kijeshi na kisiasa baina ya nchi hizi mbili."

Tags