Dec 16, 2021 03:27 UTC
  • Rais wa Russia asema uhusiano wa nchi yake na China unaleta uthabiti katika uga wa kimataifa

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, uratibu na mashauriano yanayofanywa baina ya nchi yake na China katika uga wa kimataifa umekuwa wenzo wa kupatikana uthabiti duniani.

Putin ameashiria uhusiano mzuri uliopo baina ya Moscow na Beijing na akasema: "aina mpya ya ushirikiano imeanzishwa baina ya nchi zetu, unaotokana, pamoja na mambo mengine, na misingi ya kutoingiliana katika masuala ya ndani, kuheshimu maslahi ya kila upande na kuwepo azma ya kuugeuza mpaka wa pamoja kuwa ukanda wa amani ya kudumu na ujirani mwema."

Aidha, Rais wa Russia amesema, anapanga kukutana na mwenzake wa China mjini Beijing mnamo mwezi Februari mwakani na kuhudhuria michezo ya Olimpiki ya 2022 na akafafanua kwa kusema "kama ilivyokubaliwa, tutafanya mazungumzo, kisha tutashiriki kwenye sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Baridi Kali."

Putin amekaribisha pia kuongezwa kwa asilimia 31 mzunguko wa fedha na biashara kati ya Russia na China katika miezi ya kuanzia Novemba hadi Januari.

Kwa upande wake, Rais Xi Jinping wa China naye pia ameashiria uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Russia na akasema, mashirikiano makubwa ya kisiasa yaliyopo kati ya Beijing na Moscow ni ishara ya kupanuka uhusiano wa pande mbili kwa sababu katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi mbili kilivuka dola bilioni mia moja.

Xi Jinping ameongeza kuwa, Russia na China zinatetea demokrasia ya kweli na haki za binadamu na ni mhimili muhimu wa kufikiwa mashirikiano ya pande kadhaa na kutetea usawa na uadilifu kimataifa.

Uhusiano wa Russia na China umestawi sana katika miaka ya karibuni, kwa nchi hizo mbili kufuatilia kwa pamoja malengo yao ya kikanda na kimataifa, sambamba na kuchunga maslahi ya kisiasa ya pande mbili.../

 

Tags