Dec 21, 2021 02:42 UTC
  • Ulegezaji kamba katika misimamo ya Taliban, kutoka maneno hadi vitendo

Msimamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afghanistan katika serikali ya mpito ya Taliban amesema kuwa kushirikishwa Waafghani wote katika muundo wa serikali ya nchi hiyo ni jambo la lazima.

Amir Khan Muttaqi amesema hayo katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa OIC kilichofanyika nchini Pakistan na kuongeza kuwa, Waafghani wote wana haki ya kushiriki katika tawala na serikali za maeneo tofauti ya nchi hiyo na kwamba ni jukumu la kundi la Taliban kuhakikisha jambo hilo linafanikishwa.

Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo, hivi karibuni kiongozi wa kundi la Taiban alihimiza wajibu wa kutumiwa nguvukazi ya watu welewa wa mambo katika kuendesha masuala ya sekta mbalimbali za Afghanistan. Kundi la Taliban limelazimika kuonesha mabadiliko katika misimamo yake kutokana na mashinikizo ya kieneo na kimataifa ya kulitaka liunde serikali itakayoshirikisha Waafghani wa maeneo yote na wa kada na mbari tofauti. Suala jingine ni kushinikizwa kundi la Taliban liruhusu wanawake na watoto wa kike washiriki katika masomo na shughuli za kijamii. Katika hili pia kundi hilo limeonesha kulegeza misimamo yake ya huko nyuma. Vile vile kundi la Taliban pekee halina wataalamu na watu mahiri wa kuweza kuendesha baadhi ya sekta za nchi, hivyo linalazimika kushirikisha wengine kutaka na kukataa. Pamoja na hayo lakini inaonekana kwamba matamshi ya Amir Khan Muttaqi ya kwamba kundi la Taliban linaafiki kushirikishwa watu wengine serikalini, hayakupokewa na wengine kuwa ni katika juhudi za kundi hilo za kuunda serikali shirikishi kitaifa huko Afghanistan 

Umaskini wa kupindukia Afghanistan ni katika changamoto nzito zinazoongeza mashinikizo kwa kundi la Taliban

 

Hasan Alai, mtaalamu wa masuala ya kimataifa na mhadhiri wa chuo kikuu anasema: Serikali iliyoundwa na kundi la Taliban haikushirikisha makundi wala watu wa madhehebu na mbari nyingine za Afghanistan na kwa hakika serikali hiyo ni ya kundi la Taliban peke yake.

Hata kama rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa watu walioko karibu na kundi la Taliban, hivi sasa anafanya juhudi za kulisaidia kundi hilo kupata ufumbuzi wa kisiasa kama vile kuunda baraza la Loya Jirga na kuitisha uchaguzi, lakini kundi hilo limeonesha kivitendo kuwa halina imani na mfumo wa kisiasa wa kushirikisha makundi yote na wala mfumo wa kupatikana viongozi kupitia uchaguzi na upigaji kura. Inavyoonekana ni kwamba kundi hilo limeamua kubadilisha misimamo yake katika maneno tu si katika vitendo na halijaonesha kuwa liko tayari kusikiliza vilio vya Waafghani vya kuundwa serikali shirikishi kitaifa itakayompa haki kila mtu katika uendeshaji wa taifa hilo.

Amir Khan Muttaqi, msimamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Taliban

 

Naye Abolfazl Zohrevand, mtaalamu mwandamizi na balozi wa zamani wa Iran nchini Afghanistan anasema: Taliban haijaonesha mpango wa wazi wa jinsi ya kuendesha masuala ya Afghanistan na bado kundi hilo limetekwa na aidiliojia zake za kikaumu.

Alaakullihaal, baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa kundi la Taliban wameonesha wazi kuwa kuna hitilafu kubwa za kimitazamo baina yao kuhusu ushirikiano wa kundi hilo na Marekani na pia kuhusu jinsi ya kuendesha nchi na muundo wa serikali inayopaswa kutawala nchini Afghanistan. Ijapokuwa baadhi ya wakati mrengo wa kundi hilo wenye misimamo ya wastani huwa unatoa matamshi yanayokubalika kama haki ya wanawake na watoto wa kike kupata elimu na kushiriki katika masuala ya kijamii kutokana na mrengo huo kuelewa hali halisi ya kijamii ilivyo huko Afghanistan, lakini wananchi wa Afghanistan wamethibitisha kivitendo kuwa serikali yoyote inayofanya ukiritimba wa kikundi kimoja bila ya kushirikisha watu wengine imefeli nchini humo. Kurejea kundi la Taliban katika madaraka ya Afghanistan kumetoa fursa ya kupatikana umoja wa kitaifa nchini humo kwa sharti kwamba kuundwe serikali shirikishi kitaifa na watu wote wapewe haki ya kuchagua viongozi wao. Vile vile kuweko bunge lenye nguvu la kuwawakilisha wananchi wote. Kundi la Taliban linapaswa kuelewa hilo na kutoipoteza fursa hiyo. 

Tags