Dec 21, 2021 07:42 UTC
  • UN yaipongeza Iran kwa kuwahudumia vyema wakimbizi

Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) imeipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kupokea idadi kubwa ya wakimbizi licha ya matatizo yanayoikabili na kusema imeisaidia jamii ya kimataifa.

Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Filippo Grandi ambaye alikuwa akizungumza na Waziri wa Mambo wa Ndani wa Iran, Ahmad Vahidi, ameashiria kwamba UNHCR imekuwa ikishirikiana na Iran kwa zaidi ya miaka 40 kuhusiana na masuala ya wakimbizi na kuongeza kuwa, Iran imekuwa mwenyeji mwema kwa wakimbizi wa Afganistan licha ya vikwazo vinavyoikabili.

Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa amesema, lengo la safari yake nchini Iran ni kupanua ushirikiano kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Afghanistan. Amesema wanazungumza pia na kundi la Taliban ili kuimarisha amani na utulivu nchini Afganistan na kudhibiti wimbi la wakimbizi kuelekea Iran.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Ahmad Vahidi, amezitaka jumuiya za kimataifa na Ulaya kutekeleza ahadi zao za misaada ya kifedha kwa wakimbizi wa Afghanistan. Vahidi amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haijajenga ukuta wa kuzuia wakimbizi kuingia Iran na kusema, raia wa kigeni wanaokimbilia Iran wanapewa huduma za afya na matibabu kama raia wa Iran.

Vahidi ameongeza kuwa nchi za Ulaya zinadhani kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itawapokea wakimbizi na kwa msingi huo hazina wasiwasi wa kukabiliana na wimbi la wakimbizi kuelekea mipaka yao, lakini wanaghafilika kwamba, Iran inapaswa kusaidiwa katika suala hilo.

Vilevile ameashiria sera za Marekani huko Afghanistan na kusema, hali ya sasa ya nchi hiyo imesababishwa na siasa za serikali ya Washington ambayo pia inashikilia fedha za Waafghani na kuwafanya wasumbuliwe na masaibu mengi.     

Tags