Dec 24, 2021 02:49 UTC
  • Marekani yatuhumiwa kuua watu wa Afghanistan kimya kimya

Marekani na waitifaki wake ambao waliivamia na kuikali kwa mabavu nchi ya Afghanistan kwa kipindi cha miaka 20 wameua kwa umati raia wengi wa nchi hiyo hususan watoto wadogo kwa kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi; na sasa Washington na washirika wake wanaendeleza mauaji ya halaiki na ya kimya kimya dhidi ya raia wa Afghanistan.

Shirika la habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, watu wa Afghanistan, baada ya miaka 20 ya kustahimili uvamizi wa Marekani na kukaliwa kwa mabavu nchi yao na vilevile jinai za kivita za wanajeshi wa nchi hiyo, sasa wanakasulubiwa kwa aina mpya lakini ya kimya kimya ya jinai, mauaji na vikwazo vilivyowekwa na Washington na nchi za Magharibi kwa kutumia kisingizio cha kurejea madarakani kundi la Taliban nchini Afghanistan.

Mashirika ya kimataifa yanapinga vikwazo vya Marekani dhidi ya watu wa Afghanistan yakionya juu ya uwezekenao wa kutokea janga na maafa makubwa hususan katika majira yajayo ya baridi kali nchini humo.

Sambamba na hayo taasisi za kimataifa zimeripoti kuwa, watoto milioni moja walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Afghanistan wako katika hatari ya kufa kutokana na utapiamlo na njaa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeonya kuwa, "Njaa nchini Afghanistan imefikia kiwango kisivyo na kifani."

Watoto wa Afghanistan wanasumbuliwa na njaa, utapiamlo

Itakumbukwa kuwa mwezi Agosti mwaka huu vikosi vya majeshi ya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi vililazimika kuondoka Afghanistan baada ya kundi la Taliban kuudhibiti tena mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul. Marekani na wanachama wengine wa NATO waliivamia nchi hiyo na kuikalia kwa mabavu kwa miaka 20 kwa kizingizio cha kupambana na ugaidi. 

Takwimu zinaonesha kuwa, uvamizi huo wa Marekani haukuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, madawa ya kulevya, uharibifu wa miundombinu na mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan. Katika kipindi hicho wanajeshi 2,448 wa Marekani waliangamizwa wakiwa vitani, na vilevile wanajeshi 1144 wa shirika la NATO wameuawa katika vita hivyo.     

Tags