Dec 24, 2021 07:53 UTC
  • Russia: Walioivamia Afghanistan na kuikalia kwa mabavu miaka 20, ni wajibu wao kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa, nchi zilizoivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa muda wa miaka 20 ndizo hasa zenye jukumu nambari moja la kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo.

Putin alisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari mjini Moscow na kusisitiza kuwa, wananchi wa Afghanistan wanahitajia mno misaada ya kiuchumi na kwamba nchi zenye jukumu kubwa zaidi katika jambo hilo ni za Magharibi ikiwemo Marekani ambazo zimeikalia kwa mabavu kwa muda wa miaka 20 nchi hiyo na kuvuruga uchumi wake, kusambaratisha muundo wa kijamii na kuangamiza vibaya miundombinu yake.

Rais huyo wa Russia vile vile amesema, hatua ya awali kabisa inayopaswa kuchukuliwa hivi sasa ni kufunguliwa mali za Afghanistan zilizozuiliwa na madola hayo hayo ya Magharibi hasa Marekani ambayo ndiyo yaliyoangamiza uchumi na miundombinu ya Afghanistan.

Wahanga wakuu wa ubeberu wa madola ya magharibi ni watoto wa Afghanistan

 

Ikumbukwe kuwa, nchi za Magharibi hasa Marekani zimezuia mali na mitaji ya Afghanistan kwa kisingizio cha kurejea madarakani kundi la Taliban nchini humo wakati hayo hayo madola ya Magharibi ndiyo yaliyoisababishia maafa ya hivi sasa Afghanistan na ndizo zilizohusika kwa manma moja au nyingine kurejea madarakani kundi la Taliban.

Baada ya kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa muda wa miaka 20 nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, ziliondoa ghafla wanajeshi wao nchini Afghanistan na kufungua uwanja wa kurejea madarakani kundi la Taliban tarehe 15 Agosti mwaka huu.

Madola hayo ya Magharibi yaliondoa ghafla wanajeshi wao katika hali ambayo uvamizi wao wa miaka 20 haukuwa na matokeo mengine ghairi ya uharibifu usioelezeka, kuenea vitendo vya kigaidi, madawa ya kulevya, vita, ukatili, ukosefu wa utulivu na amani na mauaji ya mamia ya maelfu ya watu mbali na idadi kubwa isiyo na kifani ya wakimbizi wa Afghanistan.

Tags