Dec 29, 2021 02:40 UTC
  • Sisitizo la Rais Maduro la kugonga mwamba siasa za Marekani dhidi ya Venezuela

Sambamba na kuendelea mashinikizo ya kisiasa ya Marekani dhidi ya taifa na serikali ya Venezuela, Rais Nicolas Maduro wa nchi hivyo amesema kuwa, taifa hilo limesimama kidete dhidi ya ubeberu na limefanikiwa kuibuka na ushindi.

Akihojiwa na Kanali ya Televisheni ya al-Mayadeen, Rais Maduro ameashiria muqawama na kusimama kidete dhidi ya hatua za chuki na uhasama wa kiuchumi wa Marekani na washirika wake dhidi ya Venezuela na kusema kuwa, nchi yetu iimekuwa ikipata maendeleo ya kweli hatua kwa hatua katika uga wa kiuchumi.

Rais Nicholas Maduro wa Venezuela amesema pia kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kulaani vikali mauaji ya kigaidi ya mwaka 2020 ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani wa Iran ambaye alikuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi na kubainisha kwamba, mauaji hayo  yaliyofanywa na Marekani ni jinai ya kuogofya. Maduro amehoji, "Je hii ndio dunia tunayoitaka, ambayo Ikulu ya White House inatoa amri ya kuuawa shujaa wa vita dhidi ya ugaidi Iraq, Syria na Lebanon?

Akizungumzia zaidi njama za Marekani dhidi ya nchi yake, Rais Maduro ameeleza bayana kwamba, nchi yake itaendelea kupinga na kulaani sera za kibeberu za Washington na washirika wake.

Rais Nicholas Maduro wa Venezuela

 

Pamoja na kuwa, kwa miaka mingi Marekani imekuwa ikifanya njama za kuwa na satua na udhibiti tena katika eneo la Amerika ya Latini, lakini katika miaka ya hivi karibuni imejikita zaidi katika suala la kuiangusha serikali ya Venezuela. Katika uwanja huo, Marekani ikiwa na lengo la kuiwekea mashinikizo ya kiuchumi Venezuela, imeiwekea serikali ya Caracaras vikwazo mbalimbali na vizito.

Kwa mujibu wa vikwazo hivyo, serikali ya Marekani imepiga marufuku kununulliwa nishati ya mafuta kutoka katika Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela kama ambavyo ikiwa mataifa mengine au mashirika ya kigeni yatatumia mfumo wa fedha wa Marekani katika biashara yao ya mafuta na Venezuela, basi yatajumuishwa pia katika vikwazo hivyo vya Washington.

Kushadidisha vikwazo, kufanya njama za mapinduzi, kuwaimarisha wapinzani wa ndani nchini Venezuela na kuwapatia bajeti na suhula wapinzanii hao, ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Washington dhidi ya serikali ya Rais Maduro. Njama hizo za Marekani zilifikia kilele pale serikali ya Washington ilipotangaza kumuunga mkono kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido na mwaka 2019 kumtambua kinara huyo wa upinzani kama Rais wa Venezuela. Pamoja na hayo, hatua na njama zote za Marekani za kutaka kuiangusha serikali halali ya Venezuela zimeshindwa na kugonga ukuta.

Kuibuka na ushindi Maduro na chama chake katika uchaguzi wa hivi karibuni na kuendelea himaya na uungaji mkono wa wananchi licha ya mibinyo yote ya kiuchumi, ni ithbati tosha ya kutozaa matunda na kufeli siasa za mashinikizio ya kiwango cha juu kabisa ya Washington dhidi ya Venezuela na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiiyo ya Amerika ya Latinii.

Kimsingi ni kuwa, licha ya kuweko mibinyo na mashinikizo hayo, lakini viongozi wa Venezuela wametekeleza sera mpya na kupanua mahusiano ya kisiasa na kiuchumi na mataifa mengine ya dunia kama Russia, China na Iran ili kuondoa mapungufu ya nchi yao na hivyo  kuleta ahueni katika masuala mbalimbali.

Pamoja na hayo, licha ya mipango michafu ya viongozi wa Marekani dhidi ya Venezuela kushindwa na kugonga mwamba, lakini wangali wanang’ang’ania kuendeleza mikakati hiyo isiyo na natija. Hii ni katika hali ambayo, katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, kuibuka na ushindi vyama vyenye mhimili wa uadilifu katika baadhi ya mataifa ya Amerika ya Latini, hususan kushinda wagombea wa vyama vya mrengo wa kushoto katika uchaguzi wa Rais nchini Chile, juhudi za Washington kwa ajili ya kulinda nafasi yake ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya eneo hilo imepata changamoto kubwa.

Juan Guaido, kinara wa upinzani nchini Venezuela anayeungwa mkono na kupatiwa misaada na Marekani

 

Inaonekana kuwa, filihali Venezuela na mataifa mengine yaliyo chini ya mashinikizo ya Marekani katika eneo la Amerika ya Latini, yataweza kuvuka kipindi hiki na kufanikiwa kutatua matatizo yanayowakabili kupitia umoja na kuimraisha ushirikiano wao wa kieneo na kimataifa. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana Rais Nicolas Maduro wa Venezuela akaeleza na kuchora taswira ya mustakabali mwema na wa wazi zaidi kwa taifa hilo katika siku za usoni.

Tags