Dec 31, 2021 02:49 UTC
  • Vifo na wasiwasi wa wakimbizi katika safari ya kuelekea Ulaya

Huku mizozo ya kisiasa na kiuchumi ikiendelea kupanuka Asia Magharibi na katika nchi nyingi za Afrika, wimbi la watu wanaotafuta hifadhi na wakimbizi barani Ulaya linaendelea kwa kasi kubwa.

Idadi kubwa kati ya wakimbizi hao wanaripotiwa kuaga dunia kwa kuzama bahari wakiwa njiani kuelekea Ulaya. Kuhusiana na suala hilo, Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa zaidi ya wakimbizi 2,500 wamepoteza maisha mwaka huu wa 2021 katika Bahari ya Mediterania wakijaribu kuvuka bahari na kufika fukwe za nchi za Ulaya. 

Kufuatia kuzorota kwa hali ya kisiasa, kuongezeka ukosefu wa usalama, vita na kushadidi matatizo ya kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni huko Kaskazini mwa Afrika na eneo la Asia Magharibi, wakazi wengi wa maeneo hayo wameamua kukimbilia Ulaya kutafuta hali bora ya maisha. Njia kuu inayotumiwa na wakimbizi na wahajiri wengi ni Bahari ya Mediterania ambayo sasa imekuwa kaburi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani kutokana na harakati za magenge ya magendo ya binadamu, boti zilizochakaa na kadhalika. Takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) zinaonesha kuwa, katika kipindi cha miaka sita iliyopita, zaidi ya wakimbizi na wahajiri 20,000 wamefariki dunia katika Bahari ya Mediterania, na Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, ameitaja bahari hiyo kuwa ni "kaburi kubwa zaidi la Ulaya."

Wahajiri wakiwa njia kuelekea Ulaya

Hii ni pamoja na ukweli kwamba, hata wahajiri na wakimbizi walioweza kufika kwenye mipaka ya Ulaya hawana hali nzuri. Kwani wengi wao wamekuwa wakingojea vibali vya kuingia katika nchi za bara hilo kwa miezi kadhaa katika hali ngumu na mazingira mabaya kupita kiasi. Italia na Ugiriki, kati ya nchi za Ulaya, zina nafasi maalumu kutokana na kuwa karibu zaidi na Bahari ya Mediterania na zinahesabiwa kuwa lango la idadi kubwa ya wahajiri na wakimbizi kuingia Ulaya. 
Meya wa Palermo katika kisiwa cha Sicily nchini Italia, Leoluca Orlando ameonya kuwa kutowapokea wakimbizi na kuwaacha wakihangaika baharini ni janga kubwa na kusema: "Siku moja Ulaya itahukumiwa kwa kufanya mauaji ya kimbari katika Bahari ya Mediterania."

Kwa sasa nchi nyingi za Ulaya nazo zimefunga mipaka yao rasmi kwa wanaotafuta hifadhi, wahajiri na wakimbizi na kuwaacha katika baridi kali na hali mbaya ya maisha; kama hali inayoshuhudiwa sasa kwenye mpaka wa Poland na Belarus. Mamlaka ya Poland imeendelea kufunga mipaka ya nchi hiyo mbele ya wakimbizi wanaotafuta hifadhi, huku mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) mjini Minsk, Belarus, akionya juu ya athari mbaya za baridi kali na mlipuko wa maambukizi ya corona miongoni mwa wakimbizi wanaohangaika katika eneo la mpaka baina ya Belarus na Poland.

Wakimbizi katika mipaka ya nchi za Ulaya

Maafisa wa Poland na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya Mashariki zimeweka kuta kwenye mipaka yao ili kukabiliana na wakimbizi hao.

Nchi za Ulaya zinawatendea vibaya wahamiaji na wakimbizi hao, wakati nyingi kati ya nchi hizo za Magharibi zimechangia katika kuibua migogoro ya kisiasa na maafa huko Asia Magharibi na barani Afrika. Ushirikiano wa nchi hizo za Ulaya na Marekani katika kuzishambulia na kuzivamia nchi kama Afghanistan, Iraq, Libya, Somalia na Syria umewalazimisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao na kukimbilia katika sehemu nyingine za dunia ikiwemo Ulaya kwa ajili ya kutafuta hifadhi na kuokoa maisha yao na familia zao. Hata hivyo Wazungu wa Ulaya na nchi za Magharibi kwa ujumla haziko tayari hata kuchukua jukumu linalolingana na mchango wao katika kuanzisha vita, machafuko na migogoro katika maeneo haya ya dunia.

Wahajiri katika eneo la English Channel

Bahari ya Mediterania, Mfereji wa Manch (English Channel) na mipaka ya nchi za Ulaya ikiwemo Poland, inaendelea kuwa machinjio ya wakimbizi na wahajiri, huku Wazungu wakiendelea kuimba nara za kutetea na kulinda haki za binadamu!!

Tags